Klabu ya soka ya Yanga imesema ipo tayari kumuachia kiungo wake Feisal Salum endapo tu taratibu za kisoka katika uhamisho zitafuatwa kama inavyopaswa.
Baada ya marejeo ya hukumu yake iliyotolewa awali kuendelea kumthibitisha Feisal Salum ni mchezaji wao halali kimkataba Yanga wamesema wanaweza kumuachia nyota huyo Mzanzibar kwa kupitia taarifa iliyotolewa na mtendaji mkuu wa klabu hiyo Andre Mtine.
Taarifa imesema ” Klabu ya Yanga inapenda kuutarifu umma kwamba ipo tayari kumuachia Feisal Salum Abdallah kuondoka klabuni kwa kuzingatia matakwa yakimkataba na utaratibu wa sheria za uhamisho za wachezaji zinazotambulika na TFF pamoja na FIFA. Ikiwa pia kuna klabu yoyote inamhitaji mchezaji huyu klabu ya Yanga ipo tayari kufanya mazungumzo wakati wowote.”
Aidha pia katika taarifa hiyo Yanga imemtaka Feisal arudi kambini haraka iwezekanavyo ili ajiunge na wenzake kuendelea na majukumu yake mpaka pale mkataba wake utakapomalizika May 30 mwaka 2024.
Yanga wamesema wapo tayari kumpokea mchezaji wake huyo baada ya maamuzi ya kamati ya sheria na hadhi ya wachezaji kumhalalisha kuendelea kuwatumikia Wananchi.