Jana Tanzania Prisons waliwalazimisha Yanga Suluhu katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam , uwanja ambao unatumiwa na Yanga kama uwanja wa nyumbani.
Suluhu ambayo Yanga hawajafurahishwa nayo kutokana na mategemeo makubwa waliyokuwa nayo awali . Yanga katika mechi mbili zilizopita wamefanikiwa kupata alama mbili pekee.
Tanzania Prisons na Mbeya City ambazo zote ni timu kutoka Mbeya katika mechi mbili zilizopita zimeifanya Yanga isolate ushindi na kuambulia alama mbili.
Baada ya mchezo huo , kocha wa Tanzania Prisons , Adolf Richard alizungumza na vyombo vya habari kikiwemo Kandanda.co.tz
Kocha huyo alidai kuwa Yanga wameshambulia na wao wamejitahidi kujilinda na kushambulia katika mchezo huo.
“Yanga wameshambulia na sisi tumejitahidi kulinda pamoja na kushambulia, wachezaji wangu wamefanya vizuri sana na wametimiza maagizo”- alisema Kocha huyo.
Kocha huyo alisema Yanga ni timu ya kawaida , siyo timu kubwa labda ni timu kongwe na kuna timu zinacheza vizuri kuzidi wao.
“Hakuna timu kubwa , ni ukongwe tu , wenzetu wamewahi kuanzishwa. Kuna timu zinacheza vizuri sana kuzidi sisi na wao ndiyo maana nasema Yanga ni timu ya kawaida “- alidai kocha huyo wa Tanzania Prisons.