Baraza la vyama vya soka ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limetangaza ratiba pamoja na makundi ya michuano ya Kagame CECAFA Cup inayotarajiwa kuanza Juni 28 hadi Julai 13 Mwaka huu jijini Dar es Salaam katika viwanja vya Azam Complex na uwanja wa Taifa.
Katika hali ya kushangaza na kushtua Miamba ya soka katika ukanda huo Simba na Yanga wamepangwa Kundi C pamoja na timu za St George ya Ethiopia na Dakadaha ya Ethiopia.
Ratiba inaonesha Miamba hiyo itakutana Alhamis ya Julai 5 katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam ikiwa ni Mechi ya mwisho ya Kundi hilo.
Aidha mpaka sasa ni jumla ya timu 11 zimeshathibitisha kushiriki mashindano hayo ambayo mwakilishi kutoka Uganda bado hajafahamika.
Kundi A | Kundi B | Kundi C |
Azam | Rayon | Yanga |
Uganda (Reps) | Gor Mahia | Simba |
JKU | Lydia Ludic | St George |
Kator FC | Ports | Dakadaha |
Ambapo kama atathibitishwa basi ataingia katika kundi A pamoja na Mabingwa watetezi Azam FC, JKU ya Zanzibar na Kator FC ya Sudan Kusini.
Kundi B linaundwa na timu za Rayon Sports ya Rwanda, Gor Mahia ya Kenya, Lydia Ludic Academy ya Burundi na Ports ya Djibouti.
Washindi wawili kutoka katika Kila Kundi pamoja na washindwa bora wawili wataungana kucheza katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza baada ya miaka mitatu kufanyika kwa michuano hiyo Kwani Mara ya mwisho ilifanyika Mwaka 2015 na Azam kutwaa ubingwa kwa kuifunga Gor Mahia ya Kenya Kwa Mabao 2-0.