Yanga SC, wameanza vibaya hatua ya makundi ya michuano ya kombe la Shirikisho baada ya kukubali kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa USM Alger, katika mchezo wa kundi D uliopigwa kunako dimba la Julai 5, 1962
Mchezo huo, uliochezeshwa mwamuzi Daniel Nii Ayi akisaidiwa na David Laryea wote kutoka Ghana, na Abel Baba hadi mapumziko USM Alger walikuwa mbele kwa mabao 2-0
Mabao hayo yaliwekwa wavuni na Ousama Darfalou kunako dakika ya nne akimalizia krosi ya Mohammed Rabie, Farouq Chafai alifunga bao la pili kunako dakika ya 34, kufuatia kazi nzuri ya Faouz Yaya
Kipindi cha pili Yanga walionekana kutaka kushambulia, lakini hali ilikuwa ngumu kwao na kujikuta wakiruhusu mabao mengine mawili
Bao la tatu, likifungwa na Abdelhame Meziane kunako dakika ya 53, akimalizia kazi nzuri ya Ayoub Abdellaoui huku bao la nne likifungwa na kipa Mohammed Amine kunako dakika ya 90, kwa njia ya penati kufuatia mlinzi wa Yanga Andrew Vicent kumchezea rafu Oussama Darfalou kwenye eneo la hatari
Hadi mwamuzi anapuliza filimbi ya kuashiria kuhitimisha mchezo huo, USM Alger waliibuka na ushindi huo wa mabao 4-0