Kuelekea mchezo wa mwisho wa kundi D wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika klabu ya Yanga imesema leo ndio mwisho wa kupokea pesa kutoka kwa mashabiki wao wanaotaka kwenda kuishangilia timu nchini Congo DR katika mchezo dhidi ya TP Mazembe.
Yanga watakua na mchezo wa kukamilisha ratiba dhidi ya TP Mazembe Jijini Lubumbashi kwani tayari wameshafuzu wao na US Monastir huku TP Mazembe na Real Bamako zikitupwa nje ya michuano hiyo.
Kuelekea mchezo huo awali tayari Yanga ilishatangaza utaratibu kwa mashabiki wake wanaotaka kusafiri kwa basi kwenda Congo kwa gharama ya laki saba pekee. Pesa hiyo itatumika katika nauli, vibali, tiketi siku ya mchezo pamoja na malazi.
Afisa habari kupitia ukurasa wake wa instagram amewaita Wananchi siku ya leo ambayo ndio mwisho waende makao makuu ya klabu wakafanye taratibu za kulipia na kupeleka shangwe nchini Congo.
“Wanachama, mashabiki na wapenzi wa klabu ya Yanga sasa tunapeleka shangwe la Kimataifa ugenini, twende Congo kwa 700,000 tu.
Kwa laki saba utapata nauli ya kwenda na kurudi, vibali (viza, vipimo vya covid, chanjo ya homa ya manjano) na tiketi ya kwendea uwanjani,” alisema Alli Kamwe.
Safari hiyo ya mashabiki wa Yanga ambapo watatumia gari la klabu itaanza siku ya kesho Machi 30 na kurudi itakua ni Jumatatu ya Aprili 3.
Endapo Yanga itapata ushindi katika mchezo huo wamwisho kwa wastani mzuri basi watamaliza vinara wa kundi mbele ya US Monastir ambae yeye anamaliza na kibonde Real Bamako.