Klabu ya Yanga imeendelea kuweka rekodi nzuri katika msimu huu wa Ligi Kuu ya NBC haswa katika eneo la mabao ambapo wao ndio timu iliyofungwa mabao machache zaidi mpaka sasa.
Yanga ndio timu iliyofungwa mabao machache zaidi katika Ligi Kuu ya NBC mpaka sasa ikiwa imebaki michezo saba pekee Ligi kumalizika. Yanga imeruhusu mabao 10 pekee katika michezo 23 waliyoshuka dimbani.
Ukuta wa Yanga unaongozwa na mlinda mlango Djigui Diarra akisaidiwa na walinzi Dickson Job, Kibwana Shomary, Djuma Shaban, Yanick Bangala, Bakari Mwamnyeto na Lomalisa Mutambala umeonekana kuwa mgumu kufikika na hivyo kuwa timu iliyofungwa mabao machache zaidi.
Klabu ya pili iliyofungwa mabao machache zaidi nyuma ya Yanga ni Simba ambao wameruhusu mabao 14 pekee katika michezo 23.
Katika timu nne zilizofanya vyema na kuruhusu mabao machache zaidi Singida Big Stars na Kagera Sugar ndio wanafunga listi hiyo. Singida wao wameruhusu mabao 19 katika michezo 24 wakati Kagera Sugar wameruhusu mabao 23 katika michezo 24.
Ligi ya NBC inaelekea ukingoni huku michezo mingi ikionekana kuwa na ushindani mkubwa mno na hivyo kupelekea ligi kuzidi kunoga na michezo kuvutia.