Katika maisha ya binadamu ni kazi ngumu sana kufika katika kilele cha mafanikio lakini ni kazi ngumu zaidi kubaki kileleni. Zipo njia ambazo humuwezesha mtu kupanda au kufanikiwa katika jambo analopanga au kulifanya lakini pia zipo njia ambazo humuwezesha mtu kuendelea kubaki kileleni isitosha zipo sababu za kumfanya mtu kuporomoka na kupoteza mafanikio ambayo alikuwa nayo awali.
Kama ilivyo mtu akipanda juu ya kitu akifika kileleni basi hana budi kushuka aidha akibaki kileleni itamlazimu kutumia gharama na nguvu kubaki alipo lakini hii haimainishi kila apandaye juu lazima ashuke.
Yanga iko katika kilele cha mafanikio, yanga iko katika nyakati za furaha za kufurahia mafanikio ya mradi wao. Kabla ya hapa yanga walijitafuta kurudisha utawala wao katika soka la ndani na nje ya nchi kwa miaka minne mfululizo bila mafanikio makubwa.
Katika misimu miwili iliyopita mradi wa Yanga waliouanzisha umezaa matunda na mafanikio makubwa baada ya kufanikiwa kurejesha ubingwa wa ligi na kombe la shirikisho yaani FA, na wamefanikiwa kufanya hivyo kwa miaka miwili mfululizo.
Isitoshe katika msimu huu ulioisha wa mashindano katika soka la kimataifa Yanga wamefanikiwa kufanya vizuri baada ya kufika fainali ya kombe la shirikisho Afrika na bahati mbaya kwao walimaliza nafasi ya pili huku wakipoteza mbele ya USM Algers ya Algeria katika mchezo wa fainali.
Mradi wa Yanga umefanikiwa baada ya kubadili mfumo wa uendeshaji kutoka mfumo wa kizamani wa kuongozwa na Mwenyekiti na Katibu mkuu na kubadilika kwenda katika mfumo wa kisasa na kuongozwa na raisi na CEO.
Uongozi imara na uletwaji wa wachezaji wazuri na waviwango vikubwa umechagiza mafanikio haya makubwa ya Yanga bila kusahau benchi la ufundi. Benchi la ufundi likiongozwa na Naserdine Nabi walifanikiwa kurejesha makali ya Yanga na kuwa timu tishio ndani na nje ya nchi.
Lakini mradi wa Yanga umepata dosari na zinahitajika juhudi za makusudi kuhakikisha mradi hauteteleki na kuanza upya tena;
▪Kuondoka kwa kocha Nabi na baadhi ya watu wa benchi la ufundi. Kocha ndiye nahodha wa timu kuondoka kwa kocha Nabi Yanga ni kama itauyumbisha mradi kama mambo yafuatayo hayatafanywa kikamilifu;
▪Kuletwa kwa kocha mpya ambaye anafanana falsafa na kocha aliyeondoka (Nabi) ili iwe rahisi kuendelea pale alipoishia mwanzilishi wake, na kama atakosekana kocha kariba ya Nabi atafutwe kocha ambaye ataendana na falsafa mama ya Yanga hii itamsaidia kocha ajaye kuendana na mazingira ya timu kwa haraka kwani wachezaji wanaifahamu falsafa ya timu hivyo itakuwa kazi rahisi kwa kocha kuingiza mbinu zake katika vichwa vya wachezaji.
▪Maandalizi ya timu kuelekea msimu mpya yaanze mapema ili wachezaji wazoee mbinu za kocha mpya na hii itasaidia wachezaji kuzizoea mbinu za mwalimu na hii itawezesha kuijenga timu vizuri na kuendelea kubaki na makali yake ya sasa.
▪Kuna wachezaji wataondoka basi mbadala wao utafutwe mapema. Wapo baadhi ya wachezaji wataachwa na timu ya Yanga, baadhi yao hawataongezewa mikataba na wengine watavunjiwa mikataba kutokana na viwango duni walivyoonesha, wengine wataondoka kwa sababu za kimaslahi na wengine watauzwa, uletwaji wa wachezaji wazuri na sahihi itasaidia yanga kuendelea kuutunza mradi wao na kubaki na ubora wake.
NB; Mtaka cha uvunguni sharti ainame.