Sambaza....

 

Ligi imesimama kwa sasa , kinachoendelea ni majadiliano ya namna gani ambavyo ligi itaweza kurudi tena baada ya kusimama kutokana na janga la Covid-19, janga ambalo limeikumba dunia nzima kwa sasa.

Wakati dunia ikiwa ndani na vitu vingi vikiwa vimesimama kwa kiasi kikubwa , tetesi za usajili zinaendelea kuwepo kutokana na vilabu mbalimbali kwa sasa kutaka kujiimarisha kwa kusajili wachezaji mbalimbali katika dirisha linalokuja la usajili.

Abdulhalim akiwa na wachezaji wenzake wa Mtibwa

Moja ya tetesi ambazo kwa sasa hivi zimekuwa kubwa kwa kiasi kikubwa ni Yanga kumtaka kiungo wa Mtibwa Sugar FC , Abdulhalim Humuod. Kiungo huyo ambaye ameonekana kufanya vizuri zaidi msimu huu akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar ya Morogoeo ameonekana kutakiwa na vijana hao wa jangwani .

Taarifa za ndani zinadai kuwa viongozi wa klabu ya Yanga wanapigana kwa sasa kuhakikisha wanapata saini ya kiungo huyo wa zamani wa Azam FC , Simba na timu ya taifa ya Tanzania pamoja na timu ya taifa ya Zanzibar , Zanzibar Heroes.

Kutokana na tetesi hizi kuenea kwa kiasi kikubwa , mtandao huu ulimtafuta Afisa habari wa timu ya Mtibwa Sugar , Thobias Kifaru ili kuweka sawa tetesi hizi ambazo zinazidi kuenea sana kwa sasa.

Thobias Kifaru ameuambia mtandao huu kuwa hakuna barua rasmi kwa sasa kutoka kwa Yanga ikimwihitaji mchezaji huyo kutoka kwenye timu ya Mtibwa ambayo makao makuu yake yakiwa kwenye mji wa Turiani , Manungu mkoani Morogoro .

“Mpaka sasa hivi hatuna barua rasmi kutoka katika klabu ya Yanga ikimwihitaji Abdulhalim Humuod kwa sababu bado ana mkataba na sisi hivo klabu yoyote inayomwihitaji lazima iwasilishe barua ya kutaka kumsajili”-alisema Thobias Kifaru.

Kifaru amedai kuwa Yanga wanakaribishwa kwenye meza ya majadiliano kama wanamtaka mchezaji huyu. “Kama wanamtaka Abdulhalim Homuod wanatakiwa waje mezani tuzungumze” alimalizia Afisa habari huyo wa Mtibwa Sugar.

Sambaza....