Najua ushawahi kuhadidhiwa kuhusu ndoto za kutisha na pengine ushwahi kuota mfululizo wa ndoto kadhaa zinazotisha.
Yanga wanaota mafanikio wako katika ndoto ya mafanikio baada ya kufanikiwa kufika hatua ya fainali ya kombe la shirikisho Afrika na kupoteza dhidi ya USM Algers ya Tunisia wakati huo Yanga wakiwa chini ya kocha Mtunisia Naserddine Nabi.
Nabi hayupo tena Yanga baada ya misimu miwili ya kuwatumikia wababe hao wa Jangwani aliamua kubwaga manyaga baada ya kushindwa kufikiana maamuzi ya kuongeza mkataba mpya na Yanga.
Yanga walimtambulisha Muargentina Miguel Gamondi baada ya kuachana na Nabi ambaye aliwapa mafanikio makubwa sana Yanga kwani alifanikiwa kuurudisha utawala wa Yanga uliopotea kwa takribani misimu minne mfululizo (2018-2021) kabla ya kupindua meza kibabe mara mbili mfululizo wakiwa na Mtunisia huyo, walifanikiwa kubeba Ngao za jamii mbili, Ligi kuu Nbc mbili na kombe la shirikisho la Azam mara mbili.
Nabi hayupo tena, tunae Gamondi na wananchi bado wako kwenye ndoto ileile tena sio ndoto ya kawaida tena bali ni ndoto ya kutisha, Wananchi wanaota mafanikio makubwa, Wananchi wanauota ubingwa wa Afrika, Wananchi wanaota kutetea vikombe vyao vyote ambavyo wamevitwaa kwa misimu miwili mfululizo, Wananchi wanaota soka safi na la kuvutia, kiujumla Wananchi wanautaka ushindi na mbeba ndoto hizo na maono yote ni GAMONDI.
Miguel Gamondi amebeba siri nzito, Gamondi amebeba ndoto za kutisha za Wananchi, Gamond anakibarua kizito cha kutafsiri ndoto hizo za kuogofya.
Mwingine atauliza nini kifanyike? Kwani ni Gamondi pekee ndo anahusika kutafsiri ndoto za Wananchi? Atafanikiwaje kuhakikisha ndoto hizi zinakuwa kweli? Apite njia gani ili afikie nchi ya ahadi? Je akishindwa kutafsiri ndoto hizo vema nani alaumiwe?
Maswali yanaweza kuwa mengi bila majibu lakini nikutoe shaka KANDANDA.CO.TZ tuko hapa kukupa majibu na kukutoa mashaka yote juu ya maswali unayojiuliza kuhusu Gamondi na Yanga yake.
Waneni walishawahi kusema kuwa “Kuupanda mchongoma si kazi bali kushuka ndio ngoma”. Yanga imekua katika kiwango bora na mafanikio katika miaka ya hivi karibuni swali ni vipi itaweza kubaki katika ubora wake uleule na kuendelea kufanikiwa. KANDANDA.CO.TZ imekuja na majibu haya;
● Ushirikiano kutoka kwa viongozi; Uongozi wa klabu ya Yanga unatakiwa kutoa ushirikiano kwa Gamondi na benchi lake la ufundi ukizingatia benchi zima la ufundi kuanzia kocha mkuu na jopo la wasaidizi wake wote ni wapya hivyo wanahitaji msaada wa moja kwa moja kutoka kwa uongozi wa klabu ili kuzikabili changamoto katika mchakato wa kutengeneza kikosi cha ushindani, Kama walivofanya kwa benchi la ufundi lililopita kwa kuwatimizia haja na matakwa yote na kuifanya Yanga kuwa bora kiasi cha kuvuma ndani na nje ya mipaka ya Tanzania basi hawana budi kumsaidia na kushirikianana na Gamondi ili Yanga iendeleze ubora na makali yake.
Waneni husema ukitaka kwenda haraka nenda pekeyako na ukitaka kwenda mbali nenda na mwenzako, ndoto za Yanga ni kufika mbali hivyo sio suala la Gamondi pekee bali uongozi pamoja nae.
● Kuutumia vyema uwanja mazoezi; Jikoni ni mahali ambapo vyakula vyote hupikwa huko basi uwanja wa mazoezi ni jikoni ambako mipango yote ya ushindi hupikwa huko, mbinu za mapambano hupikwa huko, mpango kazi hutengenezwa huko yaani ujenzi wa timu imara hufanyika uwanja wa mazoezi. Gamondi anatakiwa kuutumia vizuri uwanja wa mazoezi na kuwafanya wachezaji kuwa tayari kukubali mabadiliko ya benchi la ufundi na kubadili fikra zao na kuachana yaliyopita.
Gamondi anatakiwa kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia ili kuboost morali zao. Lakini pia katika kipindi hiki cha maandalizi ndio wakati sahihi wa Gamondi kupandikiza falsafa na mbinu zake vichwani mwa wachezaji wake ili wawe tayari, fauka na hili kama Gamondi atashindwa kuutumia vizuri uwanja wa mazoezi katika kipindi hiki cha mapumziko na maandalizi basi zile ndoto za kutisha zitamuandama kwani kikosi chake hakitakuwa fiti kupambania na kutetea mataji yake na hapo ndipo atakapotafutwa mchawi.
● Kuachana na propaganda za nje ya uwanja; Waneni husema “Zimwi likujualo halikuli ukakishwa”, soka la Tanzania kwa sasa limeandamwa na zimwi la propaganda pamoja na uzushi ambalo linatutafuna lakini hatukwishi bali yake limekua likiharibu sana mambo.
Nafahamu ya kuwa kocha Gamondi ni kocha mkubwa mwenye uzoefu wa kazi yake matarajio yangu ni kuwa anajua namna ya kukabiliana na hili, mathalani kama atamezwa na propaganda za mpira wa bongo basi atafanya kazi katika mazingira magumu yenye presha na pengine atashindwa kufanya kazi yake ipasavyo na kuifanya yanga ishindwe kuishi ndoto zake.
Mchawi wa mtu ni mtu, Gamondi na jaribio la kutafsiri ndoto ya kutisha, Endelea kuwa karibu na KANDANDA.CO.TZ usisahau kuacha maoni yako chini ya uchambuzi huu.
Je Gamomsi ataweza kutafsiri ndoto hii ya kutisha kwa wakati!?
KANDANDA.CO.TZ KARIBU KWENYE ULIMWENGU WA SOKA.