Wananchi wanaingia uwanjani leo katika mchezo wao wa tano wa kundi D wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya US Monastir katika Dimba la Benjamin Mkapa huku wakijua ni ushindi pekee ndio utawapeleka hatua inayofuata.
Yanga wanawakaribisha Watunisia hao wakiwa na kumbukumbu ya kupoteza mabao mawili kwa sifuri wakiwa ugenini na hivyo mchezo wa leo ni wakulipa kisasi pia kwa US Monastir.
Katika msimamo wa kundi D Monastir wapo kileleni wakiwa na alama 10 wakifwatia Yanga wenye alama 6 nafasi ya pili. TP Mazembe wao wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama tatu wakimzidi kibonde wa kundi Real Bamako wenye alama 2 pekee.
Yanga wanaingia uwanjani leo wakijua ni ushindi pekee ndio utakaowapeleka robo fainali kwani kama wakishinda leo dhidi ya Monastri watafikisha alama 9 na hivyo kushindwa kufikiwa na TP Mazembe. Lakini endapo Yanga watapata sare na Mazembe wakipata ushindi mbele ya kibonde Real Bamako watafikisha alama 5 na hivyo watafufua matumaini yao ya kwenda robo fainali.
Mchezo wa mwisho wa kundi hilo Yanga watamalizia ugenini Congo dhidi ya Mazembe hivyo ni vyema leo wakamalizana na Monastir wakiwa nyumbani Kwa Mkapa na kufuzu robo fainali.
Kama Yanga itapata ushindi na kufuzu leo kwenda robo fainali watakua wameweka rekodi ya kufuzu hatua hiyo baada ya kushindwa kufanya hivyo mara zote mbili walizoshiriki michuano hiyo katika hatua ya makundi.
Lakini pia itakua historia kwa nchi ya Tanzania kwani itakua ni mara ya kwanza kupeleka timu mbili robo fainali kwa wakati mmoja katika michuano mikubwa ya vilabu Barani Afrika.