Klabu ya soka ya Yanga imekutana na kibano kutoka Shirikisho la Soka Barani Afrika CAF na kulimwa faini ya mamilioni baada ya kukutwa na hatia yakufanya vitendo visivyofaa katika mchezo wake wa robo fainali kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho.
Yanga walikua mwenyeji wa Rivers United katika Dimba la Benjamin Mkapa katika mchezo wa marudiano wa robo fainali ambao ulimalizika kwa suluhu na hivyo kuwafanya Wananchi kusonga mbele lakini bado wamebaki na maumivu yakulipa mamilioni kwenda CAF.
Yanga wanapaswa kulipa fainali ya dola 10,000 ambazo ni zaidi ya milioni 20 za Kitanzania baada ya kuwasha mafataki na pia kutumia vitochi vyenye rangi katika mchezo huo uliopigwa saa moja usiku.
Pia Yanga wamekumbana na faini ya dola 25,000 zaidi ya milioni 50 za Kitanzania kwa kudaiwa kuvunja vioo vya gari la Rivers United na kupulizia dawa wakati timu hiyo ikiwa mazoezini usiku siku moja kabla ya mchezo wao.
Hivyo jumla Yanga watapaswa kulipa dola 35,000 zaidi ya milioni 70 ndani ya siku 60 baada ya maamuzi haya kufanyika kwenda CAF lakini wana nafasi yakukata rufaa.
Si Yanga pekee waliokumbana na adhabu hizo kwani timu ya Esperance de Tunis nawao wametakiwa kulipa faini ya dola 300,000 na kucheza michezo miwili ya nyumbani bila kuwa na mashabiki. Adhabu hiyo imekuja baada ya mchezo wapili wa marudiano dhidi ya JS Kabyele kutokea fujo ambazo zilipelekea mchezo kusimama kwa dakika 30.