Sambaza....

Nilikuwa naongea na rafiki yangu ambaye ni shabiki mkubwa wa Yanga ambaye huwa anapenda kujiita mwananchi.

Kwa sababu tu anaamini Yanga ndiyo timu ya wananchi na ni haki yake kujiita Mwananchi. Ushawahi kufikiria hili neno “Timu ya Wananchi” lina maana gani ?

Binafsi mara ya kwanza nilikuwa sifahamu kabisa nini maana ya neno “timu ya wananchi”. Nilikuwa najiuliza sana.

Kwanini Yanga wanajiita ” Timu ya Wananchi ?”. Kila nilipokuwa najiuliza nilikuwa sipati jibu sahihi ukizingatia kuna timu zingine tofauti na Yanga.

Hapa ndipo nilipokuwa napata ugumu wa kuelewa ukizingitia ni timu zingine zina mashabiki, swali kubwa kichwani kwangu lilikuwa, hizi timu zingine zilikuwa hazina wananchi?

Nikiwa na maana ya kuwa neno “wananchi” ni watu , kumbe nilikuwa mbali sana na ukweli wa tafasri hii ya Yanga.

Wao Yanga wana tafasri yao kabisa tofauti na sisi tunavyowaza, nilipokaa na rafiki yangu huyo ndipo nilipopata maana halisi ya neno “Timu ya Wananchi”.

Hii ni timu ya wafia damu (yani wafia damu) watu ambao wanapenda kitu kweli kweli kutoka moyoni , yani kuna watu wanaipenda Yanga kuliko wake/waume zao.

Na watu hawa ni wa kawaida sana siyo wenye kipato kikubwa, ila wanaipenda sana Yanga kuliko hata uhai wao.

Yani kwao wao Yanga ndiyo kitu cha muhimu sana. Wako tayari kulala bila kula kwa ajili ya Yanga tu. Hii ndiyo aina ya mashabiki wa Yanga ndiyo maana wakaitwa timu ya Wananchi.

Ndiyo maana ni virahisi sana kusikia Yanga inafanya changizo kwa ajili ya timu pale mambo yanapokuwa magumu.

Na hii ni kwa sababu viongozi wanaamini kuwa timu siyo yao, ni timu ya mashabiki ndiyo maana huwa wanairudisha mikononi mwao pale mambo yanapokuwa magumu.

Dismas Ten na Zahera

Ndiyo wananchi hawa sasa!, wananchi wenye timu yao kabisa. Lakini wananchi hawa wametunesha udhaifu mkubwa sana kwa viongozi wa Yanga.

Ngoja nikuambie kitu kimoja, huwa nafuatilia sana hashtaq za ndugu yangu Dismass Ten. Kuna hashtaq huwa zina maana ya kuwa Simba waliazima kombe, na msimu huu Simba wanatakiwa kurudisha hili kombe kwa Wananchi.

Hii hashtaq huwa inakuja na kupotea. Kwa kifupi ni hashtaq ya mhemuko. Lakini hashtaq hii ingetumika kibiashara kwa ajili ya kuinufaisha Yanga.

Nina maana gani?, Yanga kwa sasa inahangaika sana kutafuta pesa kwa ajili ya kuendesha timu yao. Hili halina ubishi.

Ndiyo maana wanatumia njia mbalimbali kama kuchangishana kwenye mabakuli uwanjani ili tu kupata hela tu kitu ambacho mimi nakiona ni cha kujiabisha.

Yanga wanatakiwa wawaombe Pesa mashabiki wao kibiashara siyo kwa njia hiyo ambayo mimi naiona wanajiabisha. Njia ambayo inafunga hata milango ya wadhamini kuja kuweka pesa zao Yanga.

Hii ni timu ya Wananchi, na wanaamini Simba waliazima lile kombe , wanaamini ni kombe lao kabisa.

Kwanini wasijaribu kuanzia hata kampeni kama “IT’S TIME FOR WANANCHI”. Wanaamini Simba wameazima kombe hilo.

Basi ianzishwe kampeni ambayo itakuwa inaenda na kauli mbiu ya muda wa wananchi ” ITS TIME FOR WANANCHI”.

Kauli mbiu hii iendane na bidhaa ambazo mashabiki wa Yanga wanatakiwa kununua ili timu yao iweze kupata mapato ya ziada.

Ngoja nikupe mfano mdogo, mfano kauli mbiu ikawa “ITS TIME FOR WANANCHI”. Mara nyingi saa huonesha muda.

Sasa viongozi wa Yanga wakaja na bidhaa ya saa yenye nembo ya Yanga. Saa ambayo mashabiki wa Yanga wataitumia hata kuwaonesha watu kuwa huu ni muda wao.

Kukawekwa utaratibu mzuri wa upatikanaji wa hizo saa kuanzia SAA za mkononi mpaka za ukutani. Pia saa hizi ziendane na T-SHIRT zenye kauli mbiu.

Msimu huu mwenyeji anachukua mapato yote ya mlangoni. Yanga wanatakiwa kufikiria namna ya kupata mashabiki wengi uwanjani.

Mfano hiyo kampeni yenye kauli mbiu ya Its time for Yanga ambayo itaenda sambamba na uuzaji wa bidhaa chache, kukawekwa utaratibu wa kuuza tiketi kwa mvuto.

Mfano siku moja kabla ya mechi ya nyumbani, Yanga wangetenga saa moja ambalo wachezaji watakuwa makao makuu ya klabu kwa ajili ya kuuza tiketi , kuuza bidhaa na kupiga saini kwenye jezi za mashabiki.

Mashabiki watavutika kuja kufanya hivo , mwisho wa siku Yanga itapata pesa kwa njia hii kuliko hiyo njia ya kujiabisha.

Viongozi wamelala lakini kocha wao yuko macho sana na yuko imara kuzidi wao. Ndiyo maana anafanya vizuri na timu ambayo wachezaji wake wanakaa hata miezi minne bila kulipwa mshahara kwa uvivu wa kufikiria wa viongozi.

Yanga wanatakiwa wamsaidie Mwinyi Zahera, kama Yanga ni timu ya wananchi, wananchi ambao wanapenda kitu kweli kweli.

Basi viongozi wanatakiwa wawape wananchi kitu ambacho kinaweza kuwa na kumbukumbu kwao, mtu akinunua kitu kinabaki kwake kuliko kumuomba mtu atoe hela bila kupata kitu chenye kumbukumbu.

Sambaza....