Sambaza....

Unaweza ukawa unashangaa na kichwa cha habari nilichokiandika. Unaweza ukanishangaa kabisa, inawezekana akili yako inayawaza mafanikio ya Simba msimu uliopita kwenye michuano ligi ya mabingwa.

Mafanikio ambayo kwa akili yako unaweza ukawaza kuwa ni yalikuwa mwiba wa uchungu kwa Yanga, mwiba ambao kwa wakati huu ungewafanya wafikirie namna ya wao kupambana ili kuyafikia mafanikio hayo.

Kitu ambacho kinawezekana sana, maandalizi ndicho kitu pekee ambacho kinaweza kuifanya Yanga ifikie mafanikio ya Simba ya msimu jana kwenye michuano ya kimataifa. Huu ni ukweli ulio wazi, Simba iliwafanya Yanga watamani na wao kufika sehemu kubwa.

Sehemu ambayo inafikika kwa usajili bora, kuleta wachezaji ambao wanaweza kupambana kwa ajili ya timu kwenye ligi ya mabingwa barani Afrika. Mapambano ambayo yanatengenezwa kwa maandalizi bora ndani ya timu.

Maandalizi ambayo hayapo ndani ya kikosi cha Yanga kwa sasa. Wameanza kambi ya timu yao mapema sana lakini kambi yao bado haijakamilika mpaka sasa hivi !. Yanga wamekaa Morogoro bila ya kocha wao mkuu.

Inawezekana kocha mkuu wa Yanga aliacha maelekezo ya kiufundi ya kipi kinachotakiwa kufanywa ndani ya timu kwa kocha msaidizi. Lakini uwepo wake ni muhimu sana kuliko maelekezo ambayo kocha Mwinyi Zahera ameyaacha kwa benchi la ufundi.

KMC FC walienda kushiriki michuano ya Kagame Cup kule Rwanda na ikafanikiwa kucheza michezo mitatu dhidi ya timu ngumu chini ya kocha wao mkuu Jackson Mayanja.

Azam FC pia walienda kushiriki michuano ya Kagame kule Rwanda na kufanikiwa kucheza michezo 6 ya kiushindani tena wakiwa chini ya kocha wao mkuu Ettiene Ndaragije.

Simba wako Afrika Kusini, wakiwa chini ya kocha wao mkuu Patrick Aussems na wakiwa huko watacheza mechi za kirafiki dhidi ya timu kubwa ambazo zitashiriki michuano ya kimataifa.

Mfano, Simba watacheza na Township Rollers wapinzani wa kimataifa wa Yanga katika mchezo wa awali. Baada ya hapo watacheza dhidi ya Platnumz FC, Mamelodi Sundowns, Kaizer Chiefs.

Wakati Yanga wao mpaka sasa wamecheza na timu ya Moro Kids , watacheza na timu ya kanisa na baada ya hapo tarehe nne mwezi huu wakicheza na As Vita, huku tarehe 8-11 itakuwa mechi yao dhidi ya Township Rollers, Township Rollers ambao kwenye mechi za kirafiki watacheza na Simba, Mamelodi Sundown, Kaizer Chiefs.

Sambaza....