Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameshiriki kazi za ujenzi wa uwanja mpya wa michezo wilayani Ruangwa kwa kubeba zege na matofali pamoja na wananchi.
Waziri Mkuu ambaye pia ni mbunge wa Ruangwa, ameshiriki zoezi hilo leo (Ijumaa, Mei 25, 2018) kwenye uwanja huo unaojengwa katika kijiji cha Dodoma, kata ya Nachingwea, wilayani Ruangwa, mkoani Lindi.
Akizungumza na wananchi na viongozi waliojitokeza kushiriki zoezi hilo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema ameridhishwa na kazi ya ujenzi inayoendelea hadi sasa na akatumia fursa hiyo kuwashukuru wana-Ruangwa kwa kurejesha moyo wa kufanya kazi kwa kujitolea.
“Ninawashukuru sana wana-Ruangwa kwa sababu mmeanza kufanya kazi za kujitolea, haya matofali ni matokeo ya kazi yenu, hakuna hata mtu mmoja amelipwa kwa kazi hii. Nimeambiwa yanahitajika matofali 60,000 kwa ajili ya kujenga uzio lakini hadi sasa mmeshafyatua 57,000 na zaidi, ninawashukuru sana,” amesema.
“Nimeambiwa madiwani walipiga kambi ya wiki moja hapa, Umoja wa Vijana wa CCM nao walipiga kambi, UWT walikuja kusomba matofali, watumishi wa Halmashauri nao walipiga kambi, hongereni sana kwa kurejesha moyo wa kujitolea miongoni mwa wananchi,” amesema.
Katika zoezi la leo, walijitokeza wananchi wengi wakiwemo wazee, vijana na watoto, Baadhi ya watoto walikuwa wakibeba tofali moja kwa kushirikiana wawili wawili, watatu watatu hadi wanne.
Alisema ujenzi wa uwanja huo hadi sasa umeungwa mkono na wadau mbalimbali ambapo aliishukuru Benki ya CRDB ambayo imetoa sh. milioni 15 zilizotumika kununua mifuko ya saruji 1,200; Mbunge wa Kwimba, Bw. Mansoor Shanif Hiran mifuko 1,200 ya saruji; Mtibwa Sugar mifuko 2,000 ya saruji na TFF waliotoa mbegu za nyasi kwa ajili ya uwanja huo.
Akiwa uwanjani hapo, Waziri Mkuu alipokea ahadi ya tani nne za nondo zenye thamani ya sh. milioni 10, kutoka kwa Kampuni ya Hyseas International Investment (T) Limited ya China.
Mapema, akisoma taarifa ya ujenzi wa uwanja huo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Afisa Utamaduni wa Wilaya hiyo, Bw. Simon Mwambe alisema awamu ya kwanza ya ujenzi inatarajiwa kukamilika Juni 2019 na hadi kukamilika kwake, uwanja huo utagharimu shilingi bilioni 4.64.
Alisema uwanja huo ambao unajengwa kwa kutumia vipimo vya kimataifa, ukikamilika utawezesha watazamaji 10,500 kuingia uwanjani, Pia utajumuisha michezo mingine kama mpira wa miguu, pete, wavu, mikono, kikapu na riadha.
Naye Architecture Khalid Yassin ambaye alikuwa akitoa maelezo ya ujenzi wa uwanja huo kwa Waziri Mkuu, alisema utakapokamilika, uwanja huo utakuwa na kumbi mbili za kukutania wachezaji na makocha wao, vyumba vya kubadilishia, vyoo na ofisi ya meneja wa uwanja.