Kikosi cha wachezaji 22 cha Stand United ‘Chama la Wana’ kimewasili salama Jijini Dar es Salaam Usiku wa kuamkia leo kwa ajili ya mchezo wa ligi dhidi ya Azam utakaofanyika kesho kwenye uwanja wa Azam Complex.
Kocha msaidizi Athuman Bilal amesema kikosi hicho kipo katika hali nzuri ukizingatia kuwa walikuwa mkoani Dodoma kwa kambi ya siku mbili kabla ya kusafiri Jana kuja Dar es Salaam.
“Tunaendelea kujipanga na mchezo wetu wa kesho, tunaamini tutapata matokeo mazuri ya pointi tatu, tunawaheshimu Azam na ndio maana tumetoka Shinyanga muda mrefu tukakaa Dodoma siku mbili, tunajipanga kweli kweli kwa ajili ya kupata matokeo,” Bilal amesema.
Bilal akatoa angalizo kwa waamuzi kutojaribu kuharibu uhondo wa mchezo huo kwa kuchezesha kwa haki kwa kufuata kanuni za soka, Ili apatikane mshindi anayestahili na wa halali.
Aidha amewataka wachezaji wake kucheza kwa heshima kwani mbali na Kuwa wanakutana na timu nzuri lakini pia itakuwa nyumbani kwake, hivyo ni lazima wacheze kwa nguvu na tahadhali kubwa kupata matokeo.
“Stand United hatuna mbwembwe ni timu ambayo kwa kweli tunajisifia, tunaweza kutengeneza mtu na akawa mtu kweli kweli na timu nyingine kuchukua kutoka kwetu, kesho tutawatambulisha Vijana wapya ambao naamini watakuwa hatari sana,” Bilal akizungumzia kuhusu usajili katika dirisha dogo la Usajili.
Stand United wanaelekea kwenye mchezo huo wakiwa na alama 14 wakikalia nafasi ya 13 Baada ya michezo 14 waliyocheza hadi hivi sasa.