Sambaza....

Wachezaji 20 na viongozi 13 wa klabu ya soka ya Ruvu Shooting wanatarajiwa kusafiri asubuhi ya Alhamis wakitokea mkoani Pwani kuelekea jijini Mbeya kwa ajili ya michezo miwili ya ligi dhidi ya Tanzania Prisons na Mbeya City.

Ruvu Shooting watakuwa na michezo miwili jijini Mbeya ambapo kwanza watacheza na Tanzania Prisons jumamosi ya Septemba 15 kabla ya baadae Septemba 19 kuumana na Wanakomakumwanya Mbeya City, michezo yote ikipigwa kwenye uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine.

Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire amesema wanakwenda kuwafundisha soka timu hizo mbili pamoja na kuutambulisha mfumo wao mpya wa Mpapaso Square.

“Sisi tunaweza, sasa kwa kuwa tunaweza na tunajiamini katika kuweza ndio sababu tunakuambia mpenzi na mdau wa soka kwamba Papaso Square sasa tunapeleka Nyanda za Juu Kusini, tunakwenda sasa kuwapapasa wanyakyusa” Masau amesema.

Aidha kuelekea katika mchezo wao dhidi ya Tanzania Prisons, Masau amesema timu hiyo ni kama mashemeji zao na watajisikia raha kuifunga timu hiyo kwani ni kama watani zao katika soka.

“Kwa wale ambao hawajui, Tanzania Prisons ni mashemeji zangu, na kumpapasa Shemeji kuna raha yake,” amesema.

Ruvu Shooting wameshacheza michezo miwili mpaka sasa, wakifungwa mchezo wa kwanza dhidi ya Ndanda FC ya Mtwara kwa bao 1-0 kabla ya kwenda sare ya bao 1-1 na KMC FC ya jijini Dar es Salaam.

Sambaza....