Mchezaji wa zamani wa Majimaji ya Songea, Steven Mapunda ‘Garincha’ amewatumia lawama wanachama wajuaji wa klabu hiyo kuwa ndio chanzo kikubwa kwa timu hiyo kushuka daraja msimu huu.
Mapunda ambaye msimu wa 2017/2018 ulipoanza alikuwa miongoni mwa wanaounda benchi la ufundi amesema kelele za wanachama ndio zilimeishusha daraja Majimaji kwani mbali na kushauri vibaya lakini pia walikuwa wakiponda kila kitu kizuri ambacho viongozi walikuwa wakifanya kitu ambacho anasema si kizuri.
“Unajua sababu kubwa ya Majimaji kushuka ni wanachama wa klabu, walikuwa wakipiga sana kelele na kuleta mitafaruku, wengi wanadhani ukiwa katika vilabu hivi basi kuna ulaji mkubwa lakini siyo hivyo, ona sasa wameishusha daraja timu yao wenyewe,” Mapunda amesema.
“Wakati mimi naondoka kwenye uongozi timu ilikuwa inashika nafasi ya 8, na ilikuwa na wachezaji wazuri sana, wanachama walipiga kelele na kuwafanya wachezaji wazuri zaidi ya 10 kuondoka kwenye timu, sasa hapo unadhani nini kitatokea, ndio maana umeona tumeshuka daraja,” ameongeza.
Aidha Mapunda amesema anaamini kama wanachama wataacha kasumba za namna hiyo wataweza kuisaidia Majimaji kurejea ligi kuu msimu wa 2019/2020 na zaidi pia wataweza kuisaidia na JKT Mlale ili Ruvuma iwe na timu mbili ligi kuu.
“Kama wanachama na wakazi wa Ruvuma watashirikiana kwa pamoja basi tunaweza kuzipandisha timu zetu ligi kuu, hilo linawezekana mbona baadhi ya mikoa ina timu mbili na mingine zaidi ya mbili, sisi tushindwe kwanini, lakini kwanza tuwe na ushirikiano nadhani hilo ndilo la muhimu kwa sasa,” Mapunda ameongeza.
Majimaji ambayo ilipanda daraja msimu wa 2015/2016 imekuwa ikipambana muda wote kutokushuka daraja katika misimu mitatu mfululizo lakini hatimaye wameshindwa kufanya hivyo na kushuhudia wakishuka daraja msimu huu.
Misimu yote hiyo klabu hiyo imekuwa ikikumbwa na matatizo mengi ya kiuongozi kwa wanachama ama kuisusia timu yao au kulumbana kutokana na mambo kadha wa kadha yaliyokuwa yakiikumba timu hiyo ikiwemo ukata wa fedha.