Rais wa Shirikisho la soka Barani Ulaya (UEFA) Aleksander Caferin amehuzunishwa na kitendo kilichofanywa na makocha wa timu kubwa barani humo cha kushindwa kuhudhuria mkutano wa kujadili matumizi ya Teknolojia ya Kumsaidia Mwamuzi (VAR).
Caferin amesema kitendo walichokifanya Mameneja hao ni kama dharau kwa UEFA na mpira kwa ujumla kwani mawazo yao yangewasaidia katika mkutano huo.
“Kwangu mimi sio tu kitendo cha dharau kwa mkuu wa waamuzi wa UEFA ndugu Roberto Rosetti na UEFA kwa ujumla, lakini ushawishi wa makocha ni mkubwa, kama watalalamika kufanyiwa vitendo vya uonevu na marefa ilitakiwa angalau waje na kuona washika dau wanazungumziaje kuhusu matumizi ya VAR,” Caferin amesema.
Mkutano huo ulifanyika Jumatatu na kati ya timu 10 ambazo zimefanikiwa kutinga hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ni makocha wa timu tano pekee Juventus, Paris St-Germain, Roma, Lyon na Schalke ndio ambao walihudhuria mkutano huo, huku wengine wakituma Makocha wasaidizi na viongozi wengine kuwawakilisha.
“Sasa hawatakuwa na visingizio kabisa hasa kwa wale ambao hawakutuma kabisa hata wawakilishi,” Caferin ambaye amechaguliwa kuliongoza shirikisho hilo kwa miaka mingine minne amesema.
Aidha Caferin alimtetea meneja wa klabu ya Liverpool, ambaye yeye asingeweza kuhudhuria kutokana na timu yake kuwa na mchezo wa ligi dhidi ya West Ham United siku hiyo ambapo mchezo huo uliisha kwa sare ya 1-1.
Katika raundi ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa barani Ulaya mfumo wa VAR utaanza kutumika, hatua ambayo inatazamiwa kuanza February 12 siku ya Jumanne.