“Nabii hakukaliki kwao” ni msemo ambao wahenga walisema wakiamini kuwa binadamu ana tabia ya kuzoea na kukinai, mazoea yakizidi hupelekea kuvunjiana heshima na kutoona michango ya watu katika jambo fulani.
Hata kama nabii atafanya miujiza mikubwa kiasi gani ikiwa anafanya akiwa kwao, basi ni ngumu kuaminika pengine ni kwasababu ya mazoea. Ni ngumu sana kufanikiwa ukiwa ardhi ya nyumbani (mji uliozaliwa) ikiaminika kuwa ili ufanikiwe huna budi kwenda mbali (nje).
Wageni popote pale duniani wamekuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuonyesha walichonacho kutoka kwao pengine ni sababu hatuwajui vema hivyo tunawapa nafasi ya kuwajua tofauti na wenyeji(wazawa) hatuwazingatii sababu tunao kila siku na tumewazoea.
Lakini upo usemi usemao “Zimwi likujualo halikuli ukakwisha”. Wachezaji wa Kitanzania (wazawa) wanaocheza ligi ya ndani Tanzania hawapewi thamani, hawapewi ule uzito unaostahili na pengine hii inatafsiri ule usemi wa Nabii hakubaliki kwao.
Ni kwasababu tumewazoea, ni kwasababu tunawaona kila siku na wengine tunaishi nao, wengine tunapiga nao story vijiweni wawapo mapumzikoni, lakini wazawa hawakwishi, hawapewi thamani kwenye madirisha ya usajili kama wapewavyo wageni lakini hii haiwafanyi wasiuishi mpira, hii haiwafanyi wasiendelee kupambana, bado wazawa wanapambana kukuza chapa na thamani zao licha ya kutafunwa na zimwi la kasumba ya mazoea kipindi cha usajili.
Wazawa hawapewi mikataba minono kama wapewavyo wachezaji wa kigeni. Mwingine atauliza au kuhoji kuwa wachezaji wa kigeni wanalipa kodi kubwa kuliko wazawa, vipi kwa wale wazawa wenye viwango vikubwa kuliko wageni? Vipi kwa wale wazawa wenye brand kubwa kuliko wageni?.
Kasumba ya kutokukubali vyakwetu inatufanya tutetemekee vya kigeni. Wachezaji wazawa wanaishi maisha ya kawaida sana kwasababu wanachopokea ni kidogo lakini wageni wanaishi kifahari sababu wanathaminiwa sana.
Katika kipindi cha usajili Watanzania walio wengi wanabashasha kubwa kuona sajili na utambulisho wa wachezaji wa kigeni kuliko wazawa, mchezaji mzawa akisajiliwa kwenda timu kubwa inaonekana kama hastahili badala yake wanastahili wageni, na hii inawafanya wachezaji wakizawa wanaposajiliwa na timu kubwa wabweteke wakiamini thamani yao haitaonekana hata wakifanya vizuri.
Kipi kifanyike ili kukuza hadhi na thamani ya wachezaji wazawa?
Kutafuta usimamizi bora;
Wachezaji wengi wa Kitanzania wanakosa wasimamizi wazuri (mawakala) ambao watasimama imara na kutetea maslahi mazuri ya wateja wao, badala yake wanasaini mikataba kivyao kiasi kwamba wengine wanadanganywa sababu hawajui mambo ya kimikataba na kuacha maumivu ya kudumu kwa mchezaji kwani wanatumika pakubwa na maslahi kiduchu.
Wachezaji wakizawa waende wakasome(darasani)
Ipo ile kasumba ya kuwa mchezo wa mpira wa mguu ni kwa ajili ya watu wasio na elimu, Hali ni tofauti kwasasa wasomi nao wanasakata kabumbu, kusoma kutawasaidia wachezaji wetu kuzijua lugha hivyo wakipewa mikataba wataweza kung’amua vipengele na makubaliano ya kimkataba, mfano Feisal Salum mchezaji wa Azam na mchezaji wa zamani wa Yanga aliwahi kuwa katika mgogoro na Yanga kuhusu ishu za kimkataba akidai kuwa alisaini mkataba ambao ulikuwa batili na alidanganywa na sababu ya kudanganywa alidai kuwa hakuwa akijua Kiingereza.
Mfano huu unawakilisha wazawa wengi wanaoingia mikataba na vilabu bila kujua sababu hawana elimu, hivyo rai yangu wazawa waende darasani itasaidia.
Wachezaji wakizawa wapambane wasibweteke
Ipo ile tabia ya wachezaji wakizawa kubweteka wanaposajiliwa timu kubwa, hawaoneshi ile hali ya kupambana na kupigania namba kuzisaidia timu zao bali yake wanabweteka na kufurahia kukaa benchi huku viwango vyao vikiporomoka kila uchwao.
NB: UKITAKA CHA UVUNGUNI SHARTI UINAME.