WAZIRI wa michezo Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Harrisson Mwakyembe Jumamosi iliyopita alitoa ‘matamko’ kadhaa katika siku ambayo klabu bingwa ya kihistoria nchini Yanga SC ilifanya harambee iliyokwenda kwa jina la ‘kubwa kuliko’- moja ya kauli zake alizungumzia kuhusu ‘U-LAZIMA’ wa klabu za ligi kuu Tanzania Bara kuanzia msimu ujao kutumia wachezaji wasiozidi watano kwa mchezo.
Kauli yake hiyo imezua mijadala mingi, wapo wanaoona ni sahihi na wengine wanaona jambo hilo limepitwa na wakati. Kwa mtazamo wangu, usipoegemea upande wowote kiushabiki kauli hiyo ya waziri Mwakyembe inastahili kuwa ‘sheria/kanuni’ rasmi na Shirikisho la Soka pamoja na Bodi ya ligi wanapaswa kufanya hivyo kwa uharaka.
Kuwatumia wachezaji zaidi ya watano wa kigeni kwa mchezo mmoja ni sawa na kuungamiza mpira wa nchini, kuendelea kuizohofisha timu ya Taifa, na kutoendeleza vipaji vya wachezaji wazawa. Kuuangamiza mpira namaanisha-kama klabu za Yanga, Simba SC, na Azam FC pekee zikiamua kuwatumia wachezaji saba-kumi kwa mchezo kunatengeneza tatizo.
Itazame, England katika misimu ya karibuni wamekuwa na rundo la wachezaji vijana wenye vipaji. Vijana hao wameweza kuisaidia England kufika nusu fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka uliopita nchini Urusi, na mwaka huu pia wamefanikiwa kufika hatua ya nusu fainali katika michuano ya Ligi ya mataifa ya Ulaya.
Kiubora, Ungland wana vijana waliobora lakini ‘utitiri’ wa wachezaji wa kigeni katika klabu zao kubwa nne ( Manchester United, Chelsea, Liverpool, Arsenal, Manchester City) unapelekea kukosa wachezaji bora katika nafasi muhimu.
England tangu kustaafu kwa walinzi Rio Ferdinand na John Terry wameshindwa kupata walinzi imara wa kati licha ya kwamba wana vipaji vingi kama Harry Maguire, Kelvin Tripper, John Stones asiye na nafasi ya kudumu kikosini City. Ukitazama matatizo makubwa ya England kwa sasa ni ukosefu wa wachezaji wa nafasi muhimu katika timu yao ya Taifa.
Ukitazama safu za viungo katika timu za United, Liverpool, Chelsea, City n ahata Arsenal utagundua kuwa England haina wachezaji wa kutosha katika nafasi hiyo, si kwamba wanashindwa kuzalisha wachezaji wenye ubora, hapana, wanaweza lakini tatizo kubwa ni kukosa muendelezo na uzoefu katika michuano mikubwa kwa sababu kwa sasa England haina nyota wa nafasi muhimu katika klabu zao kubwa zinazocheza kila msimu katika ligi ya mabingwa ulaya.
Leo hii wachezaji wa nafasi muhimu wa England hawatoki Manchester United, Chelsea, Liverpool, City, Arsenal Zaidi wanatoka klabu ndogo kama Tottenham , Everton na klabuni nyingine ndogondogo, je, nyota hao wanaweza kuibeba England katika michuano mikubwa?
Itazame Taifa Stars pia, leo hii wachezaji wa nafasi muhimu kama beki za kati, kiungo mchezesha timu na mshambulizi wa kati hawatoki katika klabu zetu kubwa ( Yanga na Simba) ambazo kimsingi hizi ndizo zinapaswa kuwa msingi wa kwanza wa timu ya Taifa ya Tanzania kwa sababu upo uwezekano wa wachezaji wanaochezea klabu hizo kupata michezo mingi ya kimataifa ambayo huongeza ufanisi, uzoefu, na hamasa ya mchezaji.
Leo hii Simba, Yanga kama zitashindwa kuwa na walinzi imara wazawa ni wapi tena Taifa Stars itapata msaada wa wachezaji? Tunapaswa kurudi katika sheria za kuwabana wageni na kuwaendeleza wazawa wenye vipaji kama Kennedy Juma, Salum Chuk una wengineo wanaoshindwa kuzichezea klabu kubwa kwa sababu ya wageni wenye uwezo wa kawaida kama Paschal Wawa.