Ndiyo mabingwa watetezi na wawakilishi wa Tanzania katika michuano ijayo ya CAF. Walifanya usajili, usajili mkubwa kitu ambacho ni kizuri kwenye timu yoyote ambayo inataka kushinda.
Lakini kuna baadhi ya wachezaji ambao wanatakiwa kuondoka kuanzia dirisha dogo la usajili na dirisha kubwa kwa manufaa ya vipaji vyao na kwa manufaa ya timu kwa ujumla.
Adam Salamba
Maisha yake kwenye ligi kuu yalianzia kwenye timu ya Stand United. Lipuli walimsogeza Iringa, Iringa ikawa njia ya yeye kwenda Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya au nzuri akaenda Kariakoo sehemu ambayo kuna timu kubwa mbili hapa Tanzania.
Alienda Kariakoo ambako kila jicho la shabiki hutamani kuona mchezaji akiwa kwenye kiwango kikubwa muda wote.
Jicho la shabiki wa timu za Kariakoo halina uvumilivu sana. Kwa bahati mbaya Salamba kaja kipindi ambacho kuna watu ambao ni ngumu kuwaweka benchi kutoka na mizizi ambayo wameshaiweka tayari ( Emmanuel Okwi, Meddie Kagere na John Bocco). Hivo kwa manufaa ya kipaji cha Adam Salamba na manufaa ya timu ya Simba ni bora wampeleke kwa mkopo sehemu ambayo atapewa muda mwingi wa kucheza.
Naamini kupitia kipaji cha Salamba , naamini anaweza kuwa msaada kwa baadaye. Kumweka benchi kunaweza kumpoteza, hivo ni bora kumpeleka kwa mkopo sehemu atakayocheza kwa minajili ya kumrudisha baadaye.
Mohammed Rashid
Mfungaji bora wa Prisons msimu uliopita, yupo Simba kama hayupo. Nafasi yake ni finyu sana katika kikosi cha Simba. Inawezekana yalikuwa maamuzi sahihi kwake yeye kuja katika kikosi cha Simba lakini kwa manufaa ya kipaji chake kwa nafasi ambayo anacheza ni bora dirisha dogo atafute timu kwa sababu nafasi yake inaushindani mkubwa sana.
Mohammed Ibrahim
Kwake yeye ni sahihi kuondoka pale Simba. Imekuwa ngumu kuaminika tena ndani ya kikosi cha Simba.
Kwa manufaa ya kipaji chake ni bora aende sehemu ambayo atapata nafasi ili aokoe kipaji chake ambacho kilikuwa kikubwa na msaada mkubwa msimu juzi.
Mohammed Hussein “Tshabalala”
Anaweza kutumika kama mchezaji wa akiba kutoka na wingi wa mechi. Lakini kukaa benchi kwa Mohammed Hussein ” Tshabalala” kutamsaidia yeye kurudisha kipaji chake?
Kinachomsumbua kwa sasa Mohammed Hussein ni yeye kurudisha kiwango chake.
Hawezi kurudisha kiwango chake akiwa benchi.
Ni bora kwa manufaa yake atafute sehemu ambayo atapata nafasi ya kucheza ili arudishe kipaji chake.
Munish Dida
Golikipa mkongwe , inaweza kuwa na faida kwake kuwepo katika kikosi cha Simba?, uzoefu wake ni msaada? Kikosi cha Simba hakina wachezaji wazoefu? Hapana shaka kina wachezaji wazoefu wengi kama kina Erasto Nyoni, Pascal Wawa, Emmanuel Okwi, Meddie Kagere, John Bocco.
Hivo sidhani kama Simba walihitaji mchezaji mwenye uzoefu hasa eneo la golikipa alilopo Aishi Manula.
Hivo Kuwepo kwa Dida hakuna faida kubwa kwa Simba zaidi ya kupoteza pesa za kumlipa mshahara.