Sambaza....

Ligi ikiwa imesimama kutokana na nchi kuchukua tahadhari ya kuenea kwa ugonjwa wa Corona tayari baadhi ya timu zimechukua fursa hiyo kuanza kujiimarisha kwaajili ya msimu ujao kwa kuanza kutafuta wachezaji wa kuwasajili.

Klabu kubwa nchini tayari zimeshaanza kuonyeshana umwamba katika soko huku kila timu ikitaka kujiimarisha zaidi kwa msimu ujao. Katika eneo ambalo vita inatajwa kua kubwa ni katika eneo la kiungo. Tetesi za usajili zimekua zikiwahusisha mara kwa mara wachezaji wa eneo hilo. Achana na tetesi za Yanga kutaka kumrudisha Makambo au za Simba kumtaka Shonga wa Orlando Pirates au kumrudisha Okwi tazama hapa viungo wanaotajwa katika usajili.

Sure Boy

Imeitumikia Azam fc kwa zaidi ya miaka 10 sasa lakini amekua akiambiwa ana mapenzi na Yanga kutokana na baba Mzee Salum Aboubakar kupita Jangwani. Yanga sasa wanataka kufanya kweli kwa kumshusha Jangwani ili akatengeneze safu ya kiungo na kina Niyonzima na Tshishimbi. Huku yeye mwenyewe pia huenda ukawa wakati sahihi kwake kwenda kutafuta changamoto mpya nje ya Azam fc.

Salum Aboubakar “Sure boy” akimtoka mchezaji wa Ruvu Shooting

Said Hamis Ndemla.

Mkataba wake na Simba unamalizika mwishoni mwa msimu huu, imezoeleka kila dirisha la usajili jina la kiungo huyo kuhusishwa na Yanga. Lakini safari hii huenda yakatimia kutokana na Yanga kua na nguvu ya pesa kutoka GSM huku wadau wengi wa mpira wakitamani Ndemla kuondoka Simba na kwenda kupata changamoto mpya.

Said Hamis Ndemla.

Papy Tshishimbi.

Papy ndani ya wiki mbili hizi ameviteka vyombo vya habari na mitandao ya kijamii akihusihwa na kwenda Simba lakini Yanga wakashtukia mchezo na kumuita mezani ili kuweka mambo sawa. Inasemekana alishawatajia mpaka dau viongozi wa Simba lakini kukaa kwake Yanga muda mrefu ndiko kulichofanya kubaki na kusubiria mkataba mpya na Yanga.

James Kotei

Baada ya kuachana na Simba kwa msimu mmoja tuu tayari mashabiki na wadau wa Simba wamemkumbuka kiungo huyo wa shoka. Klabu ya Simba bado inaonekana kupwaya katika eneo la kiungo mkabaji huku Mbrazil Fraga akishindwa kulitendea haki eneo hilo na hivyo kupelekea nafasi ya Kotei bado ionekane.

James Kotei (Kushoto) akimthibiti Muleka wa TP Mazembe

Benard Morrison

Baada ya kuwafunga Simba na kuwasha moto katika VPL maboss wa Simba walianza kufanya mipango ya kumsajili huku Morrison mwenyewe akikiri kufuatwa na Simba. Lakini Benard aliamua kuchagua heshima na kubaki Yanga huku akiacha kitita kikubwa cha fedha cha Simba. Inaaminika Simba walitenga dola 40,000 kwa Morrison lakini yeye akaamua kusaini Yanga kwa dola 25,000 tu.

Abdulahim Humuod

Amefunga magoli mawili mpaka sasa akiwa na Mtibwa Sugar huku akicheza kiungo wa ulinzi katika kikosi cha Wakatamiwa, amekua akihusihwa na kujiunga na klabu ya Yanga baada ya kufanya vizuri akiwa na Mtibwa. Alifanikiwa kujiunga na Yanga atakua ameweka rekodi ya kuzichezea timu tatu kubwa nchini za Simba, Azam na Yanga kama walivyofanya Mrisho Ngassa na Deo Munishi Dida.

Abdulahim Humoud “Gaucho”

Wakati dirisha litakapofunguliwa tutapata ukweli wa tetesi hizi na kuona nani atafanikiwa kuwapa kandarasi viungo hawa mafundi.

Sambaza....