Sambaza....

Wachezaji 7 hatari wa timu ya taifa ya Burundi hawa hapa.

Timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars inatarajia kujitupa uwanjani septemba 4 mwaka huu katika mchezo wa kwanza wa  kuwania kufuzu kombe la dunia kabla ya kurudiana septemba 8 jijini Dar es salaam.

Katika mchezo huo, timu zote zinaonekana kujiandaa vyema ili kuhakikishia nafasi kuelekea mchezo wa marudiano. Stars amabayo inanolewa na kocha wa muda, Mrundi, Etiene Ndayiragije inaonekena kuwa vizuri na kuwa tayari kuelekea mchezo huo.

Kocha Ndayiragije amesema kuwa, kikosi kiko vizuri kwa upande wa afya na hata uimara wa miili yao.

“ Vijana wote wameripoti, afya zao ziko vizuri, nguvu za kupambana zipo, tunaimani kila kitu kitakaa sawa…”

Kikosi cha Stars chenye wachezaji 25, wachezaji 22 tayari wako kambini huku wanne wakiwa bado hawajawasili na wanatarajiwa kufika moja kwa moja nchini Burundi wakitokea katika timu zao.

Wachezaji hao ni Mbwana Samata (nahodha), Simon Msuva, Abdi Banda, na Addi Yusuphu. Kocha Ndayiragije amedai kuwa wachezaji hawa wakubwa na anaamini huko waliko wanajiweka fiti zaidi, wanachohitaji kutoka kwake ni maelekezo tu.

Nimeona sio mbaya kama nikikusogezea wachezaji 7 hatari zaidi  kutoka timu ya Taifa ya Burundi, maarufu kama Intamba m’Urugamba kwa maana ya Wamezaji.

Lengo la kufanya hivyo ni kufanya Mwanakandanda upate kuwajua zaidi, pia hata wachezaji nao wapate kuwajua vizuri ili iwe rahisi kuwakabiri katika mechi zote mbili.

Burundi ni miongoni mwa nchi ndogo zinazounda jumuiya ya Afrika mashariki, licha ya udogo wake lakini ina historia yake mujarabu katika soka la Afrika hasa baada ya kufuzu michuano ya mataifa Africa, AFCON.

Burundi inayofundishwa na kocha Mzawa Olivier Niyungako  tangu mwaka 2016 imejikuta ikishika mkia katika msimamo wa kundi B katika michuano ya afcon 2019, Ikitoka bila alama yoyote mbele ya Guinea, Nigeria na Madagasca.

Licha ya kupata matokeo mabovu katika michuano ikiwa ni sawa na timu ya taifa ya Tanzania, Burundi sio ya kubeza hata kidogo kwani ina vijana wana vipaji, ina wachezaji wengi wa nje na wenye uzoefu.

Hawa hapa ndio wachezaji hatari zaidi katika kikosi hicho, ambacho kinaonekana kuwa na morali zaidi na kutaka mafanikio katika siku za hivi karibuni.

1. FISTON ABDUL RAZAK

Huyu ni mshambuliaji anayeichezea klabu ya JS Kabylie ya Algeria. Huyu ni miongoni mwa wachezaji waliofanikisha kuipeleka Burundi katika michuano ya Afcon.

Licha ya kutokupachika bao lolote katika michuano hiyo lakini, Fiston anaonekana kuwa ni mchezaji hatari na wa kuchungwa zaidi kwani ni mzuri wa kushuka kuchukua mipira kutoka chini na kuanza kasi ya kushambulia, maana yake ni mzuri akicheza namba 10, au “false 9’, ni mzuri wa kupiga pasi ndefu za kutua mguuni, pia anajua kukaba kuanzia juu “pressing”, kukokota mipira na kupiga vyenga.

Udhaifu wake mkubwa ni mipira ya juu, kwa maana bado hayuko vizuri katika matumizi ya vichwa kufunga mabao. Hupenda kushamnbulia kwa kutokea katikati na ni mara chache kumkuta anatokea pembeni.

2. ENOCK SABUMUKAMA.

Huyu ni miongoni mwa vijana wenye viwango vikubwa na kutumainiwa nchini Burundi. Enock ni kiungo anayekipiga na Zesco united ya Zambia. Ana miaka 23 pekee, lakini kazi yake uwanjani usipime.

Hucheza katika nafasi mbalimbali uwanjani lakini mara nyingi hucheza kama kiungo mshambuliaji  na hata Mshambuliaji.

Kutokana na nafasi yake uwanjani, Enock ni mzuri katika kujenga mashambulizi, kutoa pasi za msingi na hatari, kupiga krosi na hata kukokota mpira na kupiga vyenga.

Ni mzuri kwa mipira ya hamsini kwa hamsini (1×1), mpira humtii pindi anapouamrisha (ball control) pia anajua kupiga ‘Tackling’ zenye mafanikio. Huyu ni wa kumchunga sana, sio wa kumpa nafasi ya kupiga shuti, kwa kuwa anajua vyema kulenga lango.

Udhaifu mkubwa wa kiungo huyu, ni kwamba mipira mingi hupotelea kwake, hii ni kutokana na kukaa na mpira muda mrefu.

3.KARIMU NIZIGIYIMANA.

Huyu ndiye beki wa kutumainiwa wa Burundi na Vipers ya Uganda. Kiasili ni beki wa kati lakini pia hata shavu la kulia anasukuma bila kukwama. Nizigiyimana ni miongoni mwa mabeki wenye uzoefu mkubwa kwa Tanzania ni sawa na Erasto Nyoni.

Sifa kubwa ya beki huyu, ni kujua njia nzuri ya kuanzisha mashambulizi kutoka nyuma, anajua kupiga pasi za aina zote, fupi na ndefu, anajua kuipandisha timu pale anapohitajika kufanya hivyo.

Ni mzuri kusafisha mipira ya hatari “clearance”, ni mzuri kukokota mpira,  na kupokonya.

Udhaifu mkubwa wa beki huyu, ni mipira ya hewani, yaani krosi za vichwa tu utakuwa umempatia, ni adimu sana kupiga ‘tackle’ na ikafanikiwa, hajui kupiga krosi, udhaifu mkubwa zaidi aliokuwa nao ni kupoteza mpira kwa adui.

Kwa aina hii ya uchezaji wa beki huyu, Samata na wenzake wanaweza kutuhakikishia ushindi endapo kama watakaba kuanzia juu kwa kasi ‘pressing’  ili kumtia presha na kufanya makosa.

4. HUSSEIN SHABANI.

Huyu ni miongoni mwa washambuliaji wenye uwezo mkubwa sana kutoka klabu ya Ethiopia Bunna na timu ya taifa ya Burundi. Hussein mwenye miaka 29 anaweza kucheza vema katika nafasi ya ushambuliaji na hata kiungo sifa kuu aliyokuwa nayo ni uwezo wa kupiga mashuti.

Mshambuliaji huyu ni mzuri akitokea chini katika eneo la viungo kwenda kushambulia. Uzuri huu unachagizwa na uwezo wake mkubwa katika matumizi ya nguvu na kupiga mashuti kutoka mbali.

Huyu ni mzuri sana kukaba kuanzia juu, ni mzuri kuingilia mchezo, na hata kupiga ‘tackle’ zenye mafanikio. Hii inamaanisha kuwa, mabeki wa Stars wakawe makini katika kupiga pasi mpenyezo hasa kupitia katikati, kwani huenda zikakutana na huyu kiumbe.

Udhaifu wake mkubwa ni katika mipira ya hamsini kwa hamsini, lazima afanye madhambi, mipira mingi pia hupotelea kwake, kwa kushindwa kupiga pasi sahihi na hata kupokonyewa miguuni, sio mzuri sana wa kupiga vyenga na hata kukokota mpira, mwisho kabisa, Husseni ana rekodi ya kutenda madhambi mengi.

5. GAEL BIGIRIMANA.

Ukiniambia nikutajie kiungo fundi zaidi katika timu ya Burundi nitakwambia Guel Bigirimana. Ukiniuliza ni kwanini nitakupa sifa chache tu lakini huenda sababu kubwa ni mimi mwenyewe kuwapenda ‘Viung- Punda’.

Bigirimana ni fundi na mtawala wa kudumu wa dimba la chini na la juu katika timu ya taifa ya Burundi na klabu ya Hibernian ya Scotland, kiufupi huyu jamaa ni ‘Box to box midfielder’.

Kiungo huyu ni fundi wa kupiga pasi za aina yote, fupi na ndefu, pasi muhimu na zenye madhara ‘key passes’, mara nyingi huhakikisha safu ya ulinzi inabaki salama kwa udhamini wa mguu wake wa kulia, ni mara chake hupanda kushambulia.

Ni mzuri wa kuingilia mashambulizi ya timu pinzani, kuokoa mipira ya hatari na kuimiliki mipira inayozagaa langoni mwake.

Udhaifu wake ni mipira ya krosi, na kupiga pasi ndefu sahihi. Licha ya kuwa mzuri wa kulilinda dimba la chini lakini sio mzuri sana wa kucheza ‘Tackle’ zenye mafanikio, pia hupoteza mipira akikutana na timu yenye presha kubwa.

6. PIERRE KWIZERA.

Kutoka nchini Oman katika klabu ya Al-Orouba huyu ni kiungo wa ulinzi wa kutumainiwa na Warundi katika harakati za taifa hilo kufuzu michuano ya kombe la Dunia nchini Qatar.

Huyu unaweza muita ‘pass master’,anajua kupiga pasi za aina zote zikiwemo zile za maudhi. Anajua kupiga pasi ndefu katika pande zote za uwanja, pasi za kudondosha, kiufupi ana jicho la mwewe.

Kwenye kupiga ‘tackle’ zenye mafanikio hapa ndio nyumbani, ni mzuri kupokonya mipira katika eneo lake la hatari, kukokota na kuingilia mashambuzili. Sifa zake za kiuchezaji kama za N’gholo Kante wa Chelsea.

Udhaifu wake mkubwa ni mipira ya hamsini kwa hamsini, mipira ya hewani na hata ardhini, kwa maana hana ujuzi wa kutosha katika hili.

7.OMAR NGANDU.

Ulishawahi kusikia neno ‘beki jiwe’? ni huyu jamaa. Ni Mrundi anayekipiga katika klabu ya AS Kigali ya Rwanda. Ni miongoni mwa mabeki wa kati wa kutumainiwa wa nchi hiyo.

Ngandu ni mzuri wa kupiga pasi fupi fupi na kuiongoza safu ya ulinzi kuwa imara kwa muda wote. Omar hupenda kucheza kama beki wa kati kwa kupande wakulia, ana rekodi nzuri za kupiga ‘tackle’ zenye mafanikio, kuokoa mipira ya hatari na  kukokota mipira ya hatari langoni mwake.

Sifa kuu aliyokuwa nayo amabyo mabeki wengi wa Burundi hawana ni mipira ya vichwa, Omar ni mzuri kupiga vichwa na hata mipira ya hamsini kwa hamsini ya juu na ya chini.

Sifa hizi zinamfanya Omar kuwa ni beki aliyekamilika, ana mapungufu machacvhe ambayo kukosa uwezo wa kupiga vyenga, kupiga mipira ,mirefu na kupiga pasi za muhimu (sifa hizi sio muhimu sana kwakuwa ni za washambuliaji na viungo).

Kutumia wachezaji hawa, wenye viwango vikubwa katika timu, kocha wa  Burundi hupenda kutumia mfumo wa  4-2-3-1, huku eneo ambalo linaonekana kumsumbua ni eneo la ulinzi. Katika mechi nyingi alizocheza kuanzia michezo ya kufuzu Afcon na hata Afcon yenyewe amekuwa kibadilisha safu ya ulinzi kwa takribani kila mchezo.

Mchezaji pekee ambaye amekuwa akipewa nafasi katika takribani kila mchezo katika nafasi ya ulinzi ni Fredric Nsabiyumva anayechezea klabu ya Chippa United inayoshiriki ligi kuu nchini Afrika ya Kusini.

Wengine ni golikipa Jonathan Nahimana wa Vital’O,Mshambuliaji Mohammed Amissi wa klabu ya Jong Heracles ya Uholanzi na Saido Berahino Mshambuliaji kutoka klabu ya SV Zulte Waregem ya Ubelgiji.

Wachezaji wa Burundi wapo wengi wazuri tena wengi wao hucheza nje ya nchi. Narudia tena Burundi Sio nchi ya kuidharau wala kubeza  kwani ina wachezaji wenye vipaji vikubwa.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Taifa Stars.

Sambaza....