Sambaza....

Fuatilia uchambuzi wangu wa wachezaji 11, ambao wangekuwa bora zaidi kama wasingejiunga na vilabu vya Yanga SC na Simba SC. Wachezaji hawa nikama walidumbukia katika pipa lenye maji ya moto zaidi chini baada ya kuvutiwa na joto la juu tuu. Walipotea!


#01; SAID MOHAMED ‘NDUDA’

Ningeweza kumpanga Shaaban Kado au Beno Kakolanya katika nafasi hii, lakini namchukulia Nduda kama kielezo sahihi.

Baada ya kuibuka kama mmoja wa magolikipa bora katika ligi kuu Tanzania Bara msimu wa 2010/11 akiwa na timu ya Majimaji FC, Said alifanya makosa kwa kuichagua Yanga katika usajili wa Juni 2011.

Yanga ndiyo timu iliyokuwa ikimwaga pesa kama ‘njugu’ wakati huo, na ilikuwa tayari na golikipa bora raia wa Ghana, Yaw Berko.

Nasema, Nduda alikosea kujiunga na Yanga wakati huo kwa sababu mabingwa hao wa kihistoria wa Tanzania Bara licha ya kuwa na Berko pia walimsaini aliyekuwa kipa bora wa ligi kuu msimu wa 2010/11, Shaaban Kado.

Nduda alijiunga sambamba na Kado na wawili hao wakawa wasaidizi wa Yaw. Aliondoka Yanga baada ya kuruhusu magoli manne kati ya matano katika kichapo cha ‘karne’ katika Dar-Pacha, May 7, 2012 wakati Yanga ilipochapwa 5-0 na m,ahasimu wao Simba.

Youth Rostand

Baada ya kuondoka Yanga, nyanda huyo alitangatanga kabla ya misimu mitatu iliyopita kuibuka tena na kuwa kipa bora nchini akiwa na kikosi cha Mtibwa Sugar FC.

Katikati ya mwaka 2017, Nduda alishinda tuzo binafsi ya golikipa bora wa michuano ya COSAFA Cup huko Afrika Kusini licha ya kuichezea Taifa Stars katika mchezo mmoja tu.

NAAMINI alikuwa na nafasi kubwa ya kujijenga kimpira kama angeamua kurudi Yanga ambayo ilikuwa imewapoteza walinda mlango wake Ally Mustapha na Deo Dida, lakini ajabu Nduda akaungana na Aishi Manula katika kikosi cha Simba.

Baada ya Yanga kushindwa kumrejesha, Nduda ikakimbilia kumsaini Mcameroon, Youthe Rostand na nyanda huyo akaishia kukaa benchi Simba hadi alipoondoka kwa mkopo Januari hii na kujiunga Ndanda FC.

Miezi minne ya Nduda ndani ya Ndanda inadhihirisha ni kwa kiasi gani nyanda huyu alivyo na uwezo wa juu, lakini hatakwenda kuiwakilisha Taifa Stars katika fainali za CAN2019 huko Misri baadae mwezi ujao kutokana na kujali zaidi pesa na si mchezo wake.

#JE nduda alipata pesa iliyomkidhi wakati alipotoka Majimaji na kujiunga Yanga mwaka 2011? na je, amepata pesa iliyomtosheleza wakati alipoamua kuicha Yanga na kuichagua Simba miezi 20 iliyopita?

#Nampanga golini kipa huyo katika kikosi changu cha nyota walioboronga katika usajili na kujidumaza katika soka lao.

#Nani utampanga beki ya kulia? Upande wangu nafikiria kumpanga Salum Kanoni, au Geofrey Taita!

Sambaza....