Ligi kuu soka Tanzania bara hatua ya lala salama imeendelea tena leo kwa michezo mitatu ya mapema, ambapo Singida united ya kutoka mkoani Singida (wababe wa Yanga) imeangukia pua baada ya kuchapwa kwa 1-0 na timu ya soka ya Lipuli FC katika mchezo uliofanyika kwenye uwanja wa Samora mjini Iringa.
Bao pekee la Lipuli FC katika mchezo huo limefungwa na Malimi Busungu katika dakika ya 17 ya mchezo huo ambao ulikuwa mkali na wa kuvutia katika dakika zote 90.
Mechi nyingine kali imepigwa katika uwanja wa Mwadui Complex mkoani Shinyanga, ambapo katika mchezo huo wenyeji timu ya soka ya Mwadui FC wamecharazwa bila ya huruma kwa mabao 3-1 na timu ya soka ya Stand United ‘Chama la wana’.
Mabao ya Stand United katika mchezo huo yamefungwa na Tariq Seif katika dakika ya 51, Sixtus Sabilo katika dakika ya 61 na Hamadi Ndikumana ‘Katauti’, wakati bao pekee la Stand United likifungwa Abdallah Seseme katika dakika 76.
Mbao 2-2 Majimaji
Katika uwanja wa CCM Kirumba, Majimaji wakitoka nyuma ya mabao mawili kwa bila wamefanikiwa kulazimisha sare ya mabao 2-2 dhidi ya Wenyeji timu ya soka ya Mbao FC.
Mabao yote ya Majimaji yamefungwa na Marcel Boniventure katika dakika ya 81 na 90 wakati mabao ya Mbao yakifungwa na Boniface Maganga katika dakika ya 60 na 62.
Mechi za Kesho:
Simba SC vs Tanzania Prisons -Taifa, Dar es Salaam.
Kagera Sugar vs Mtibwa Sugar – Kaitaba, Kagera.
Ndanda vs Ruvu Shooting – Nangwanda Sijaona Mtwara