Timu ya soka ya waandishi wa habari za michezo imefanikiwa kuibuka na ushindi mbele ya timu ya Unitalent katika mchezo mgumu wa kirafiki uliopigwa hapo jana.
Mchezo huo ulipigwa katika Dimba la Bora Kijitonyama na Wanahabari kuibuka na ushindi wa bao mbili kwa sifuri bila tabu yoyote.
Goli la kwanza la Wanahabari lilifungwa na Juma Ayo akipokea pasi safi kutoka kwa Issa Mbuzi kabla ya Mbwana Mshindo kufunga bao pili kwa shuti kali ndani ya kipindi cha kwanza.
Katika mchezo huo timu ya Unitalent ilizawadiwa penati na mwamuzi lakini uimara wa mlinda mlango wa Wanahabari Abuu Mwakyoma ulizima ndoto za Unitalent walau kupata bao la kufutia machozi.
Mpaka mpira unamalizika dakika tisini Unitalent hawakufanikiwa kuliona lango la Wanahabari lililokua chini ya walinzi Marko Mzumbe, Tony Kinunda, Toby Sebastian na Issa Mbuzi.
Unitalent hawakuishia tuu kufungwa mabao mawili lakini pia waliteseka uwanjani haswa katika eneo la kiungo ambalo kwa timu ya Wanahabari likikua chini ya Moland Wilbert akifanya kazi nzuri akisaidiwa na Mselemu Kandanda.
Ni mara ya pili sasa timu ya Unitalent inashindwa kupata matokeo mbele ya Wanahari, mwaka jana timu hizi zilipokutana mchezo ulimalizika kwa sare ya mabao mawili kwa mawili.
Mchezo huo ulihudhuriwa na waandishi wengi wa habari za michezo kama Charles Abel, Ahmed Ally, Anderson Chicharito, George Job, Abdul Mkeyenge na Anuary Binde.