Sambaza....

Kikosi cha wanarambaramba Azam FC jioni ya leo kimefanya mazoezi yake ya kwanza toka walipotoka kupokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa wapiga debe Stand United siku ya Jumapili katika mfululizo wa ligi kuu soka Tanzania Bara.

Azam ambao wamerejea jana wakitoka Mkoani Shinyanga wameanza mazoezi hayo wakiwa katika maandalizi ya kucheza na wanalizombe Majimaji mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa Azam Complex Mei 11, 2018.

Akizungumza na mtandao huu, afisa habari wa Azam FC Jaffary Idd Maganga amesema wanajua ugumu wa mchezo huo na ugumu wa timu ambayo wanaenda kukutana nayo na ndio maana wameanza mazoezi hayo mapema ili kukusanya alama tatu.

“Tumeanza mazoezi rasmi kujiandaa na mchezo wetu unaofuata dhidi ya Majimaji ya songea, kwa hiyo walimu wanaiandaa timu kuanzia leo kwani Majimaji ni moja ya timu bora Tanzania Bara  licha ya kwamba matokeo yao sio mazuri sana, inahangaika isishuke daraja, kwa hiyo unapokutana na timu kama hizi mchezo unakuwa mgumu,” Maganga amesema.

Baada ya kichapo kutoka kwa Stand United, Azam wameendelea kuikamatia nafasi ya pili wakiwa na alama 49 huku wakiwa wameshacheza michezo 27, ili hali Majimaji wao ambao wamecheza michezo minne bila kupoteza wanashika nafasi ya 13 wakiwa na alama 24.

 

Sambaza....