Sambaza....

Wiki imeisha na wiki mpya imeanza bila ya Simba kucheza mchezo wowote wa ligi kuu Tanzania kwa kisingizio cha kujiandaa na michuano ya kimataifa.

Linaweza likawa jambo jema kwa Simba kwa sababu wanapata muda mrefu wa kupumzika kabla hawajakutana na Nkana FC ya Zambia katika michuano ya ligi ya mabingwa barani ulaya.

Wachezaji wake hawatokuwa na uchovu kuelekea kwenye mechi hiyo, watakuwa na nguvu nzuri ya kupambana kwa sababu ya kupata muda mwingi wa kupumzika.

Hata pia kiakili watakuwa vizuri, inawezekana kabisa kama wangecheza mechi ya ligi kuu Tanzania na kwa bahati mbaya wakapoteza basi kiakili wangeathirika kuelekea kwenye mechi hii ya kimataifa.

Na pia timu inakuwa na muda mwingi wa kufikiria mchezo mmoja wa kimataifa, timu inatumia muda kujiandaa na mchezo huo pekee.

Wanatumia muda mwingi hata kuwatazama Nkana FC wanavyocheza kupitia vyanzo mbalimbali ambavyo wanakuwa wamevipata.

Akili zao kwa sasa zinafikiria kitu kimoja, nacho ni hiyo mechi pekee. Kwa kifupi Simba inafaida kubwa kwa sasa kutocheza mechi za ligi kuu Tanzania kuliko hasara.

Kwa sasa kuna hasara chache sana kuliko faida, lakini kwa baadaye kuna hasara kubwa sana kuliko faida kwa sababu Simba itakuwa na mrundikano wa mechi nyingi za viporo kwenye ligi.

Ndiyo muda ambao watatumia kucheza mechi mpaka 3 ndani ya siku saba, na wakati mwingine itawalazimu wao kusafiri mpaka mikoani.

Hapo uchovu wa mrundikano wa mechi nyingi ambazo watakuwa wanacheza ndani ya wiki moja ili tu kukamilisha ratiba ya mechi za viporo.

Pia watakuwa na uchovu wa kusafiri mara kwa mara mikoani huku wakipata muda mchache wa kupumzika.

Hapa ndipo kutakuwa na asilimia kubwa kwa Simba kuweza kupoteza dira yao ya kutetea ubingwa na ikizingatia kipindi ambacho anaanza kucheza mechi zake za viporo kitakuwa kipindi ambacho timu nyingi zitakuwa zinataka alama ambazo zitawasaidia kubaki ligi kuu au kuendelea.

Hivo hata uzito wa mechi husika unakuwa mkubwa kuliko kipindi hiki ambacho ligi haijamaliza hata mzunguko wa kwanza.

Kwa hiyo ingekuwa ni busara kwa uongozi wa Simba kukataa mechi za viporo kipindi hiki ambacho timu inashiriki michuano ya kimataifa.

Inaweza ikawa faida kwao kwa kipindi hiki lakini kwa baadaye itakuwa ngumu kwao, kwa sababu ya mrundikano wa mechi ambazo utawafanya hata matayarisho kuanzia kwenye akili watakuwa hafifu.

Sambaza....