Klabu ya soka ya Villarreal imemfuta kazi kocha Luis Garcia baada ya siku 50 tu toka alipopewa kibarua cha kuinoa timu hiyo ambayo haijashinda mchezo wowote kwenye michuano ya ligi kuu nchini Uhispania toka mwishoni mwa mwezi November mwaka jana.
Klabu hiyo imetangaza kumfuta kazi kocha huyo Jumanne hii na kwamba watamtangaza kocha mpya ndani ya masaa machache kutoka sasa.
“Tunapenda kumshukuru Garcia kwa kazi yake, kujitoa na ubora wake, tunamtakia kila lenye kheri katika kazi yake mpya na maisha yake mazima ya ukocha, kocha mpya wa timu atatangazwa masaa machache kutoka sasa,” ilisema taarifa ya klabu hiyo.
Luis Garcia alichukua nafasi ya Javi Calleja tarehe 10 Disemba mwaka jana, akishinda mchezo mmoja pekee kwa mabao 2-0 dhidi ya Spartak Moscow kwenye michuano ya Uropa Ligi, lakini tangu kipindi hicho timu imetoka sare michezo minne na kupoteza michezo miwili ya ligi na kuondolewa na Espanyol kwenye mashindano ya Copa del Rey, na kuifanya timu kufikisha michezo nane bila ushindi.
Kwenye msimamo wa ligi, Villarreal wapo katika
nafasi ya 19 katika ligi yenye timu 20, alama tano kutoka katika nafasi salama
ya kutoshuka daraja, na mechi ijayo watacheza na Espanyol siku ya jumapili.