Katika Kipindi cha Usajili Timu hushusha Vyuma; Azam FC, Simba, Yanga, Singida Fountain Gate kila Moja inajitahidi kuwa na kikosi Bora kwa Msimu Ujao. Katika sajili zote, swali kubwa na la Msingi ni Je sajili Mpya ni sajili sahihi? Je wachezaji hao watafiti na kuperform Vizuri kwenye timu husika?
Timu kama Simba bila shaka wanamkumbuka mchezaji kama Ismael Sawadogo, Victor Akpan, Nelson okwa, Augustine Okrah, Mohamed Watara, na Dejan Geojevic; Yanga wanamkumbuka Lazorious Kambole, Twisila Kisinda, na Gael Bigirimana. Hawa Wote ni Wachezaji waliosajiliwa kisha wakashindwa Kuperform kwa Msimu Husika kiasi cha timu kuamua kuwaacha.
Unaweza Ukaona kawaida; lakini sio kawaida; Yaani timu kama Simba Imeshawapa Mkono wa kwaheri wachezaji watano waliojiunga Msimu; Balaa ni kwamba; ni wa kimataifa; maana yake kuna shida Mahali.
Mashabiki, Viongozi na hata wadau wa soka hawana la kujitetea zaidi ya kusema, Usajili Ni Kamari, unaweza kupatia, au unaweza kukosea, Unayemsajili anaweza Fanya Vizuri au akashindwa kufanya Vizuri. SI KWELI, NI UONGO, NI KUJIDANGANYA, NI KUKATAA MAKOSA NA KUTOKUBALI KUTAFUTA SULUHU YAKE.
Wengi wanasema, Mchezaji anaweza kuwa Bora katika Timu Fulani, lakini akawa Mbovu katika Timu Nyingine; tena Bila sababu za Msingi kama Majeraha. Narudia tena ‘Kuna shida Mahali’ Leo nipo hapa Kukuonyesha shida yenyewe ni Ipi, ipo wapi na Inaweza Kutatuliwaje?
Kwa Utafiti wangu Mdogo nilioufanya; Sijaona Timu hata Moja Nchini inayokwepa Changamoto hii; Kila timu usajili kwake ni kamali; Kamali isiyo na uhakika wa matokeo chanya; kila timu haina huu utaratibu nitakao kwambia; maana yake timu zitabadilishana Vilio Tu. Ambatana nami hadi mwisho; hakikisha Unaelewa vizuri Uchambuzi huu; najua kupitia wewe mabadiliko yanaweza Kutokea.
December 2018, Akitokea Katika klabu ya Leipzig ya Ujerumani, Muaustralia Ralph Hasenhuttl anafanikiwa kuweka alama ya kimapinduzi katika Klabu ya Southampton ya Uingereza, alama ambayo itakumbukwa milele.
Alama hii ndio nataka kuitumia leo kuzifundishia Klabu zetu nchini; alama hii ni Kijitabu kidogo kwa Muonekano lakini kikubwa kimawazo kilichosheheni Taswira ya Klabu kwa Malengo ya muda Mfupi na Mrefu. Kitabu hiki Naweza kiita BASE PLAN, lakini wenyewe Waingereza wanakiita SOUTHAMPTON PLAYBOOK.
Timu za Tanzania zinakosa BASE PLAN; THE PLAY BOOK; Simba hawana, Yanga hawana, Azam nao hawana na ndio maana Usajili wao ni wa Hovyo.
Twende tukaone suluhu za Sajili za kamali kwa Vilabu Vyetu, SIMBA na Yanga zikiwa kama Mifano.
Kiufundi Kosa kubwa kwa Vilabu vyetu linaanzia pale kunapokosekana kwa Utamaduni wa KIufundi ambao utatumika kama Msingi mkuu wa kiufundi kutoka Levo ya juu hadi ya chini. Hapa huhusisha
- Staili ya uchezaji,
- Mbinu
- Falsafa na
- Viwango vya Kitabia kwa kila mchezaji kutoka Timu Kubwa hadi timu za levo za chini.
Hii ndio sababu ya Kusema Simba na Yanga zinazokosa Base Plan, kwa maana huu ndio Msingi wa kila kitu ndani ya Klabu. Je nini kifanyike? Kuna Vitu Vikuu Vinne; Pigia mstari, VITU VIKUU VINNE. Nakuhakikishia Vitu hivi, timu yoyote ikiviweka sawa kama BASE PLAN yake, Ndani ya Miaka Mitatu, Ubingwa wa Afrika Huu hapa; Zile kelele za Kupata hasara, KWISHINEHI, ZILE changamoto za Kusajili MAGALASA, ZITAISHIA HAPO, USAJILI HAUTAKUWA KAMALI TENA, UTAKUWA NI SAYANSI YA KITABUNI; KILA ANAYESAJILIWA LAZIMA AFANYE VIZURI; je ni Vitu gani hivyo twende ndani zaidi…
- Kuwe na STAILI moja ya Kiuchezaji (falsafa)
Watu wanaitamka Falsafa ya Klabu kama kitu kidogo sana; wanaitamka kirahisi Mno. Falsafa ni Msingi wa mafanikio ya klabu, Falsafa Ni kama Utamaduni wa kiuchezaji. Huu ni msingi ambao klabu yoyote duniani inayoendeshwa kisasa iko Nao.
Falsafa inaelekeza staili ya Kiuchezaji, Mbinu za Kiuchezaji, aina ya wachezaji wanaotakiwa katika kila nafasi ya Kiuchezaji na sifa zao za Kiufundi, Falfasa hujibu maswali yote ya jinsi timu inavyotakiwa kucheza katika Kanda zote za Uwanja.
Hii Faida yake Ni nini? Simba na Yanga kila Msimu zinashiriki zaidi mashindano Matatu, maana yake kwao ni Kama Project. Kuwa na wachezaji wanaofiti kwenye Falsafa Fulani huisaidia timu kuwatumia wachezaji husika kiufasaha lakini pia kwa faida kubwa kuliko kila mwaka kubadili Falsafa na wachezaji wanaofiti kwenye Falsafa husika.
Kiujumla Mabadiliko ya mara kwa mara huzaa hasara kubwa kwa Vilabu Vyetu, hasara ambayo wengi hawataki kabisa kuiona kama hasara. Kwa Mfano, Klabu ya SImba mwaka 2019/20 ilisajili wachezaji 14, wannne ndio walifanya Poa, wengine Kamali; mwaka 2020/21 ilisajili wachezaji 10, Wanne wakafanya tena poa, wengine ikaendelea kuwa kamali; mwaka 2021/22 ilisajili wachezaji 11, watano wakafanya Poa, wengine Kamali, mwaka 2022/23 ilisajili wachezaji 12, waliofanya Vizuri ni Moses Phiri, Saido Ntibanzonkiza na Jean Baleke, wengine wote kamali.
Hii inaletwa na nini? Kila msimu timu inabadili kocha, kila kocha huja na falsafa zake, ‘automatic’ ana wachezaji wake wanaofiti, na wale waliosajiliwa Msimu uliopita hujikuta hawafiti. Matokeo yake ni kila Mwaka kusajili Rundo la wachezaji na kuwaacha, klabu inapata hasara. ingekuwa na falsafa Moja, ingesajili wachezaji wanaofiti kwa Falsafa husika, hata ikitokea kocha akatimuliwa, basi Wachezaji wapo, na kocha mpya atakayekuja atafuata Falsafa iliyopo na wachezaji wake.
- Kuwafundisha makocha.
Huenda ni Ngumu sana kumpata kocha wa falsafa yako Uliyoichagua; lakini ni rahisi mno kumpa kocha kile unachokitaka kutoka kwake kisha akakifuata. Hapa namaanisha Klabu lazima zipate makocha ambao wapo Flexible ili kuendana na mahitaji ya KLABU kifalsafa.
Na hapa nieleweke Vizuri, hii haichagui kocha, Makocha wote waliopo ndani ya Klabu lazima wawe Waumini wa Falsafa ya Klabu. Ilitokea pale Simba, enzi za Pablo Franco, Kocha mkuu anafundisha soka la Nguvu lakini mazoiezi wanawafanyishwa wachezaji hayawafanyi waendane na aina ya soka la kocha Mkuu.
Kwa timu ya Hivi ni ngumu sana kupata matokeo. Hivyo kila kocha, kuanzia Mkuu na benchi lake lote la ufundi, lazima Wafuate Mahitaji ya kifalsafa.
- Soka la Vijana
Timu yenye ‘Base Play’ huwa na Ufanano wa kila Kitu kuanzia levo ya Juu kwa maana timu ya Wakubwa na tImu zote za Vijana katika Umri mbalimbali. Jiulize; Simba au Yanga timu zao za Vijana zinafundishwa Flasafa safa na Timu za wakubwa? Robertinho anatakafundisha Soka la kasi, gengen Pressing, Suleimani Matola kule kwenye Timu za Vijana anafundisha Falsafa gani? ‘Possessional Play’.
Nenda Azam FC, Nenda Yanga, utakutana na Jibu Moja tu, kuna tofauti za Kifalsafa kutoka Timu kubwa hadi timu zingine. Kwanini hii ni Muhimu? Kuwa na falsafa Moja inarahisisha ‘Flow’ ya Wachezaji kutoka timu za Vijana hadi timu Kubwa.
Hii inamaanisha Kijana akionyesha uwezo katika Timu B, ana nafasi kubwa ya kufanya Vizuri Pia akipandishwa timu A kama kutakuwa na Ufanano wa Kifalsafa. Jiulize swali lingine. Ni vijana wangapi hupandishwa kutoka Timu B kuja timu A kila mwaka? Suluhisho ni kuwa na Ufanano wa Kifalsafa KWA vikozi Vyote vya timu.
- Kutumia Falsafa husika kama KICHUJIO kwa kila anayeingia ndani ya klabu.
Usajili wa Simba na Yanga ni kutokana na Kiwango cha Mchezaji fulani katika mechi fulani. Timu haina kichujio kingine zaidi ya Takwimu za Msimu lakini pia Kiwango cha MECHI Fulani. Hivyo ndivyo walivyosajiliwa wakina Victor Akpan, Perfect Chikwende, Lazarius Kambole, Twisila Kisinda na wengine hata wa msimu huu. Hii ndio sababu ya kupata wachezaji wanaofeli kila msimu; hii ndio sababu ya kusema ujali ni ‘Kamali’ Timu zetu zinakosa kichujio muhimu sana cha Kifalsafa.
NINI TIMU ZETU ZIFANYE?
Timu zetu Mtu muhimu anaitwa ‘Mkurugenzi wa Ufundi’. Huyu ndio injini ya Timu katika masuala ya Kiufundi; ana kazi nyingi sana; hivyo hawezi kuwa PEKE YAKE; bali ni Kitengo ambapo ndani yake kuna wataalamu mbalimbali wanaofanya jambo moja. Kiufupi hii ni Idara.
Katika timu nyingi duniani huyu ni daraja kati ya Kocha kwa maana ya benchi la Ufundi na Uongozi wa Klabu; Huyu husimamia vitengo vyote katika timu na kuhakikisha vinafanya kazi zao Kwa usahihi na Ubora Mkubwa.
Huyu ndiye anayehusika na Usajili wa Wachezaji na Watu wa benchi la Ufundi kama Makocha, Huyu hushughulikia masuala ya Wachezaji kama Mikataba yao na hata wale waliopo kwingine kwa Mkopo.
Mbali na majukumu hayo; jukumu kubwa na la msingi ni kuendeleza na Kusimamia Falsafa ya Klabu bila kusahau Tamaduni Zake.
Katika timu kama Simba au Yanga; Ukimuacha Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wa Klabu huyu ndiye Mtu mkubwa Zaidi anayesimamia masuala ya Ufundi na Kuhakikisha timu inapata mafanikio kwa kila Msimu. Mkurugenzi wa ufundi mara zote Hufanya kazi kwa matokeo ya kesho kwa maana Kutengeneza faida kubwa Baadae.
Timu yenye Mkurugenzi wa ufundi haiwezi kutimua Kocha kila baada ya Msimu Mmoja; lakini pia haiwezi Mleta Kocha Anayefundisha Falsafa tofauti na Falsafa Mama ya Timu; Kufanya hivyo ni hasara.
Hapa namaanisha Hatua ya kwanza kwa Klabu zetu ni kumpata Mkurugenzi wa Ufundi atakayefanya kazi kwa Uhuru na katika ukamilisho wake. Vuta picha, timu zetu zikafanya kama Hivi, niambie baada ya miaka Mitano zitakuwa wapi?.