Wakati Ulimwengu wa soka ukiwa unatizama namna jua linavyozama kwa mkali Christiano Ronaldo aliyetamba kwa zaidi ya miaka 10 kwenye soka, ulizo la wengi limekua juu ya nani atakua mrithi wa ufalme wake kwenye Kandanda.
Huu umekua ni mjadala usio na majibu ya moja kwa moja kwani kila mdau wa mpira ana maono na mtazamo wake binafsi.
Ni dhahiri kuwa inafikirisha na inahitaji sababu kibao kumtaja mchezaji yeyote yule anayechipukia kuwa ndiye mrithi wa Ronaldo hapo baadae.
Katika pita pita zangu mitandaoni, nimekutana na ‘Status’ ya mmoja kati ya wajuzi wa soka akiwa kaweka picha mbalimbali za kijana Mbappe na kuandika hivi “BAADA YA CR7 TUNAYE MBAPPE”, imenifikirisha saana.
Ni mara nyingi kinda huyo anayecheza kunako klabu ya Paris Saint German (PSG) na timu ya Taifa ya Ufaransa amekua akiiga na kufanya yale yanayofanywa na mkongwe Christiano, kama namna ya kushangilia, uvaaji na hata uchezaji kwa namna flani.
Hii ni taswira kamili kuwa Mbappe anataka kuwa kama Ronaldo, kwa maana hiyo kioo cha Mbappe ni CR7, ataweza kweli?
Ikumbukwe kuwa mpaka sasa CR7, ndiye kashikilia rekodi ya kuwa mwanasoka mwenye mabao mengi katika michuano ya UEFA akiwa na magoli 128, zaidi ya vikombe vikubwa 30, pia ndiye mwenye mabao matatu kwa mchezo ‘Hat-tricks’ mengi zaidi tangu rekodi zianze kutunzwa ye anazo 56.
Huyu huyu Ronaldo pia ndiye anaongoza kwa kuwa na ‘hat-trick’ nyingi kwenye michuano mikubwa ya UEFA akiwa nazo nane, tena jamaa ni mchezaji pekee kufunga zaidi ya mabao 60 kwenye michuano yote katika miaka minne mfululizo, na ni moja ya wachezaji waliocheza mechi zaidi ya 1000, kwenye maisha yao, aisee jamaa anarekodi kibao tuishie hapo kwanza🙌🏽, je Mbappe ataweza?.
Kylian Mbappe leo hii ana miaka 21, na ameshatwaa kombe la Dunia na mataji mengine tofauti akiwa na timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu yake ya Paris Saint Germain FC (PSG), umri wake nguvu, uwezo na juhudi ni silaha tosha ya kuzifikia ndoto zake.
Ni mnafiki pekee asiyependa maendeleo ya binadamu mwenzie, kama mdau wa soka amemtabiria Mbappe kuwa CR7, ajeye mimi ni nani nipinge?.
Kila la kheri Mbappe katika kuzifikia ndoto zako.