Ndoto ya Manchester City ya kutwaa mataji manne msimu huu imezimwa usiku wa kuamkia leo baada ya kukubali kutolewa kwenye michuano ya ligi ya Mabingwa Ulaya na vijana wa Tottenham kwa bao la ugenini.
Manchester City ambao tayari walikuwa na taji la kombe la Ligi, walikuwa na matumaini makubwa ya kufudhu hatua ya nusu fainali hasa baada ya bao la Raheem Sterling katika dakika za majeruhi lakini teknolojia mpya ya kumsaidia mwamuzi (VAR) ikalikataa bao hilo na kuwafanya Tottenham ambao walikuwa nyuma ya mabao 4-3 kufudhu hatua ya nusu fainali kwa mtaji mzuri wa bao la ugenini.
Kocha wa Manchester City Pep Guardiola amesema namna walivyotolewa ni namna ya kikatili sana lakini hawana namna nyingine zaidi ya kukubali hali hiyo na kubadilisha mawazo yao kwenye mataji mengine mawili yaliyobaki.
“Ni ngumu, ni namna ya kikatili lakini tunalazimika kukubali, tumepambana sana miezi tisa il nina washukuru sana wachezaji wangu kwa namna walivyojitoa, miezi kumi kwa ajili ya Ligi kuu England ambayo bado ipo mikoni mwetu sasa, tunatakiwa kuchukua taji hili,” amesema.
Baada ya Tottenham kupata ushindi wa bao 1-0 nyumbani Juma moja lililopita ilikuwa ni lazima kwa Manchester City kupata ushindi mnono ili kujihakikishia kufudhu hatua inayofuata.
Katika mchezo wa Jumatano hii ilishuhudia mabao matano yakifungwa katika dakika 21 za mwanzo ambapo Manchester City waliingia kwa kasi na kupata bao la mapema katika dakika ya nne kupitia kwa Raheem Sterling kabla ya Heung-Min Son kufunga mawili dakika ya saba na ya kumi, naye Bernardo Silva akaongeza la pili kwa Manchester City dakika ya 11 na Raheem kufunga bao la tatu dakika ya 21.
Mabao mengine katika mchezo huo yamefungwa na Sergio Aguero kwa upande wa Manchester City na Fernando Llorente kwa upande wa Tottenham.
Sasa Tottenham atacheza nusu fainali na Ajax kwa kuanzia nyumbani April 30 mwaka huu.