Mwanasheria mkuu na Waziri wa Sheria nchini Ghana Gloria Akufo amesema hakuna ushahidi wa moja kwa moja kumtia hatiani Bosi wa zamani wa shirikisho la Soka nchini Humo Kwesi Nyantakyi.
Akufo amesema mpaka sasa Hakuna ushahidi wa moja kwa moja ambao unamtia hatiani Nyantakyi ambaye alinaswa na Camera za Mwandishi Anas Aremeyaw Anas akichukua Rushwa ya Dola 65,000 kwa ajili ya udhamini wa ligi kuu nchini humo.
“Sijapokea nakala Zozote ambazo zinamtia hatiani Nyantakyi, nadhani uchunguzi unaendelea kufanyika upande wa mashtaka watakapomaliza na kunitumia nitaangalia kuna nini,” amesema.
“Unahitaji kuwa na ushahidi wa kutosha ili kuisogeza mbele kesi kwenye mahakama, lakini mpaka sasa sijapokea ushahidi wowote kutoka kwa walalamikaji wala wachunguzi, na kama Ofisi yangu haitapokea chochote basi hatuwezi kufanya lolote,” ameongeza
Nyantakyi ambaye amekuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini Ghana toka 2005 alichaguliwa mwaka 2016 kuwa mjumbe wa kamati ya FIFA lakini video za kichunguzi za Mwandishi Anas Aremeyaw Anas zilimlazimu kujiuzulu kwa nafasi zote hizo.