Unakifahamu kikosi cha mwaka cha shirikisho la soka duniani (FIFA) kilichotokana na kura za watu wenye ushawishi katika soka zaidi ya 1000 duniani kote? Sawa! nitakurudisha nyuma kidogo hadi septemba 24, mwaka huu, sherehe hizo zilizofanyikia London Uingereza zilimuweka De Gea, Marcelo, Dan Alves, Sergio Ramos, Raphael Varane, Edin Hazard, N’golo Kante, Luka Modric, Christiano Ronaldo, Kylian Mbappe na Lionel Messi kuunda 11 bora ya dunia.
Achana na hao wote, mimi nimevutiwa zaidi na beki wa kulia wa Paris Saint- Germain (PSG) na timu ya taifa ya Brazil, Daniel Alves da Silva maarufu kama Dani Alves.
Imekuwa ni kawaida kwake kujumuishwa katika vikosi vya mwaka kwa bara la ulaya na hata dunia kwa ujumla kupitia FIFA. Hadi sasa Alves amejumuishwa katika kikosi cha dunia mara 8, mwaka 2009,2011,2012, 2013, 2015,2016,2017, na 2018 pia amejumuishwa katika kikosi cha mwaka cha bara la ulaya mara tano yaani mwaka 2007, 2009, 2011,2015, na 2017.
Kinachomuweka kwenye ramani ni staili yake ya uchezaji ambayo ndio staili ya kisasa kwa wachezaji wa aina yake. Alve ni beki wa kulia, anapanda na kushuka “Wing-back”. Kupitia hiki unaweza ukajua kuwa, jukumu la mabeki wa pembeni kwa mpira wa kisasa ni kuzuia, kulinda na kushambulia kwa wakati mmoja.
Sifa nyingine, Alves ana kasi “pace”, stamina, kushambulia akitokea pembeni “overlapping” na uwezo mkubwa wa kuumiliki mpira na hiki kinamfanya aweze kucheza namba zaidi ya moja , kama vile kiungo au winga. Alves yuko vizuri kwa kupiga krosi, mipira yake mingi huwa ina macho ya kumuona straika, na kutengeneza nafasi nyingi za magoli. Pia ni mzuri katika mipira ya kutenga nje ya 18 “Long-range set-pieces”.
Sifa zake hizo katika uchezaji zinamfanya Alves kucheza kwa mafanikio makubwa katika klabu zote alizopitia kuanzia mwaka 2000. Hadi sasa amepita katika vilabu 5 yaani klabu za Bahia, Sevilla, Barcelona, Juventus na sasa yupo PSG tangu mwaka 2017.
Tuachane na huyo Mbrazili, turudi nyumbani Tanzania, na tushuke mitaa ya Msimbazi na kumuangazia beki wake wa kulia (usajili mpya), Zana Oumar Coulibaly mwenye miaka 26.
Coulibaly amejiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili kama mchezaji huru kwa mkataba wa miaka miwili yaani kuanzia mwaka 2018 hadi novemba 28 mwaka 2020.
Coulibaly mwenye uraia wa nchi mbili , Burkina Faso na Cote d’Ivoire amechezea katika vilabu mbalimbali kabla ya kutua msimbazi, amecheza African Sports msimu wa 2015/16 na ASEC Mimosas wa 2017/18 zote za Cote d’Ivoiremsimu na kisha kujiunga na Simba kama mchezaji huru.
Usajili wa Coulibaly umekuja baada ya beki tegemezi wa wekundu hao, Shomari Kapombe kupata majeraha katika kambi ya timu ya taifa nchini afrika ya Kusini, katika maandalizi ya kufuzu AFCON mwakani. Kuumia kwa Kapombe kumeifanya Simba iingie kichwa kichwa na kumnasa Coulibaly akiwa mchezaji huru.
Tangu atue Msimbazi amecheza michezo miwili pekee, mmoja wa ligi dhidi ya KMC na mwingine ni wa kombe la TFF (Azam Sports Federation Cup) dhidi ya Mashujaa ya mkoani Kigoma.
Katika mchezo wa kwanza dhidi ya KMC Simba iliibuka na ushindi wa goli 2-1. Goli hizo ziliwekwa kimyani na Adam salamba na kiungo Said Hamis Ndemla za mwanzoni.
Kiwango cha Koulibaly VS KMC.
Kiwango chake kilibadilika kadri dakika zilivyokuwa zinakatika. Mabadiliko hayo yalikuwa ni hasi. Katika kipindi cha kwanza, koulibaly alikuwa akipiga krosi zilizokuwa zikidokea eneo hatari la KMC. Katika kipindi chote cha kwanza, Koulibaly alikuwa na akili ya kushambulia tu, yaani akiupata mpira ni kupiga mbele.
Krosi zenye kuzaa mabao mengi ni zile za kwenda karibu na mwisho wa uwanja au eneo la 18 la mpinzani yaani zinapunguza umbali kati ya mshambuliaji na lango la mpinzani na kuwa ni rahisi kufunga, krosi hizi zinaweza zikawa za juu kwa matumizi ya vichwa au za chini lakini Coulibaly alishindwa kufanya yote. Anavyoonekana hayupo vizuri katika suala ya kasi katika ushambuliaji (pace and overlapping).
Kipindi cha pili, Coulibaly alipotea kabisa, upande wake uligeuzwa kuwa uchochoro, alionekana kushindwa kufanya jukumu lake mama la ulinzi. Mipira mingi ilikuwa ikiokolewa na Paul Bukaba Bundala ikitokea katika eneo lake.
Akienda kushambulia, anakwenda jumla jumla. Ni mzito kurudi baada ya kushambulia, hii ilifanya idadi ya mabeki katika safu ya ulinzi ya Simba kupungua, ukilinganisha na idadi ya washambuliaji wa timu pinzani wakiungana na viungo wao.
Koulibaly VS Mashujaa Fc.
Katika mchezo huu, Simba walilala kwa goli 3-2 na kutolewa katika mashindano hayo ya ASFC. Lakini miongoni mwa sababu za magoli hayo ni Coulibaly kushindwa kutekeleza majukumu yake ya awali na asili.
Katika kipindi cha kwanza kama kawaida yake huanza kwa kasi, akiendelea kutia matumaini. Kipindi cha kwanza alicheza vizuri japo kasi yake wakati wa kushambulia ilikuwa ndogo kiasi cha kutowatisha mabeki wa pembeni wa Mashujaa.
Utabaini udhaifu wa Coulibaly, wakita Simba ikiwa inashambuliwa. Wakati wa mashambulizi beki huyu huwa hayupo katika eneo lake analopaswa kuwa yaani haendani na kasi ya mchezo, na hii inafanya washambuliaji kucheza wakiwa huru wakiwa eneo la Coulibaly kwa sababu mwenyewe hayupo. Kiufupi unaweza ukasema, wakati Simba inashambuliwa, Coulibaly huwa anashambulia !
“…mpira ukiwa upande mwingine, labda tuseme upande wa mashariki kwenye “high pressure” yeye anakuwa ni mwepesi sana kukaa kwenye “low pressure” ambapo wachezaji wa timu pinzani hawapo “ Maneno ya Mwalimu Kashasha baada ya mechi.
Unajua, aina ya uchezaji wa safu ya ulinzi ni kusaidiana majukumu, yaani akipitwa beki wa kulia, beki wa kati atakuja kusaidia katika eneo la pembeni wakati huohuo huyu beki wa kulia, anatakiwa aingie ndani kuchukua nafasi ya beki wa kati alieenda kumsaidia katika eneo lake na wakati beki huyo anaenda kufanya “recovery” eneo la kati lazima aende akilenga kumkaba mtu maalumu au kuziba nafasi fulani. Hiki ndicho alichokuwa akikifanya Hassain Kessy akiwa Yanga na Nkana, na inamtofautisha yeye na Kapombe na hata Asante Kwasi.
Hadi sasa Coulibaly ameonyesha udhaifu mkubwa kiasi kwamba hawezi kuziba pengo la Shomari kapombe, Kapombe mwenye kila aina ya sifa za kuwa beki bora wa kulia Tanzania. Anaweza kushambulia,anakaba, analinda, ana kasi kupitia pembeni ana sifa zote za Dani Alves.
Kwa staili ya uchezaji wa Koulibaly yaani sawa na nusu ya Kapombe bado hana makali ya kuziba pengo lake. Napata shaka sana juu ya usajili wake, maana naona hastahili kuchezea klabu kama Simba yenye malengo ya kubeba ndoo klabu bingwa Afrika, huku ikimtegemea yeye kama mbadala wa beki bora Shomari Kapombe.
Najiuliza, hivi kile huwa kinasemwa na msemaji wa Simba, Haji Manala, kuwa Simba inasajili wachezaji wa kimataifa sharti wawe wanachezea timu zao za taifa hivi kilikuwa na maana au ilikuwa ni kuwapumbaza mashabiki wa Simba na wadau wa Soka nchini?
Usajili wa Coulibaly unanikumbusha, wakati nipo mkoani, nilikuwa nikiambiwa, ukiwa Dar na ukaamua kununua simu, hakikisha unapewa Simu na wala si kipande cha sabuni. Yaah! Niliambiwa wanatabia ya kuchukua hela baada ya kukuonyesha simu yenyewe kisha wanakwambia ngoja tuiweke kwenye boksi lake, kumbe kwenye boksi wanaweka sabuni ukienda nyumbani kuifungua unakuta ni kipande a sababu tena cha shilingi mia mbili.
Ni sawa na kilichoikuta Simba. Unadhani Coulibaly anaweza muweka benchi Nicolus Gyan? Vipi kapombe?
Kwa mujibu wa kocha wa Simba, Patrick Aussem anamtetea Koulibaly kuwa kabla ya kusajiliwa na Simba hakucheza kwa muda wa miezi mitano kwahiyo anahitaji muda wa kuwa timamu. Hoja yake ni ya msingi lakini swali la msingi, je Simba iliyopo katikati ya vita ilikuwa inamuhitaji mchezaji wa sampuli yake? aje kufufukia Simba?. Jibu ni hapana.
Naijibia Simba, kuwa ilikuwa inahitaji mchezaji atakayekuja kuziba pengo la Shomari Kapombe na kuongeza ushindani katika nafasi ya beki namba mbili. Lakini kwa aliyesajiliwa ni bora hata waliokuwepo.
Akiendelea kucheza kama anavyocheza inabidi asahau kwa muda kupata namba katika kikosi cha kwanza, hii ni kwa manufaa ya klabu.