Njia ya kuelekea Ubingwa wa Kombe la Dunia mwaka 1950 ilikuwa ya aina yake; badala ya kuchezwa katika hatua ya mtoano, hatua ya awali ya makundi ilifuatiwa na hatua nyingine ya makundi kwa timu zote kucheza kwa pande zote (round-robin group).
Timu nne za mwisho zilikuwa Brazil (nchi mwenyeji na ndiyo timu iliyoongoza kwa kuwa na magoli mengi kutoka katika hatua ya makundi, wakitoka kupata ushindi dhidi ya Mexico na Yugoslavia, na sare dhidi ya Switzerland), Uruguay (ambao walijikuta wakicheza mechi moja tu katika kundi lao, waliichabanga mabao 8–0 Bolivia, kundi lao lilitakiwa liwe na timu tatu, Uruguay yenyewe, Bolivia na Ufaransa lakini Ufaransa walijitoa baadaye hivyo ikachezwa mechi hiyo moja tu), Hispania (ambao walishinda mechi zao zote tatu za hatua ya makundi, dhidi ya Uingereza, Chile na Marekani), na Sweden (ambao walifuzu mbele ya mabingwa watetezi wa dunia, Italia, na Paraguay).
Brazil walishinda mechi zao zote mbili za kwanza kwa ushindi mujarabu, wakiichapa Sweden 7–1 na Hispania 6–1 na kuongoza kundi kwa pointi nne kuelekea mechi ya fainali. Brazil walikuwa wamekamilika katika mashindano haya walikuwa na nguvu na kutawala dimbani- walifunga magoli 23 katika mechi 5 za mashindano walizocheza kabla ya mechi yao ya mwisho na Uruguay. Wakiwa na pointi tatu, Uruguay walikuwa ndiyo wanaofuatia katika nafasi ya pili, ingawa ilibidi watoke nyuma wakiwa wamefungwa 2–1 na kutoka sare ya 2–2 na Hispania, kabla ya kuwachapa Sweden mabao 3–2, huku bao la ushindi likiwa limekuja katika dakika tano za mwisho kabla ya mchezo kumalizika.
Katika mechi kati ya Sweden na Hispania, Sweden ilihitaji ushindi mbele ya Hispania, ili kumaliza katika nafasi ya tatu ya Kombe la Dunia. Hispania wangejihakikishia nafasi ya tatu kwa kupata sare, au hata kumaliza wa pili kama wangeshinda, kwa kujumlisha na kipigo ambacho Uruguay wangefungwa, jambo ambalo lisingewezekana baada ya kuwa Brazil wamefunga mabao 13 katika mechi mbili zilizopita.
Mechi kati ya Brazil na Uruguay, kwa namna moja, ingeamua hatima ya ubingwa; ushindi ama sare ingewapatia Brazil ubingwa, wakati ambapo Uruguay walitakiwa washinde mechi ili kupata ubingwa. Mchezo huo mara nyingi huwa unaorodheshwa kama fainali ya Kombe la Dunia la mwaka 1950, ingawa kusema kweli hii haikuwa hivyo; ila ilikuwa ni mechi ya kuamua mshindi wa mashindano hayo.