Msimu jana Antonio Conte alikuwa anatumia mfumo wa 3-4-3, mfumo ambao ulimpa uhuru wa kuwatumia Kante na Matic kama viungo wa kati.
Matic alicheza kama box to box midfielder na alifanikiwa kupiga pasi za mwisho za magoli zaidi ya saba katika ligi kuu ya England peke yake.
Baada ya msimu jana kuisha, Antonio Conte aliamua kumuongeza Bakayoko kutoka Monaco na kumwachia Matic kwenda Manchester United.
Bakayoko alikuja Chelsea kukiwa na matumaini makubwa sana ya yeye kufanya vizuri kulingana na kiwango chake kizuri alichokionesha akiwa na Monaco.
Lakini tofauti na matumaini makubwa ya watu wengi, Bakayoko amekuwa mchezaji ambaye ana kiwango cha chini sana. Amekuwa akionesha makosa mengi ndani ya mchezo. Yafuatayo ni makosa ya kiufundi ambayo Bakayoko amekuwa akiyafanya ndani ya uwanja.
Msimu jana Antonio Conte alikuwa anatumia mfumo wa 3-4-3, lakini msimu huu alibadirika na kuanza kutumia mfumo wa 3-5-2, mfumo huu unamwezesha kuanza na viungo watatu wa kati, mara nyingi huwa wanacheza Kante, Bakayoko na Fabregas/Drink-Water. Katika mfumo huu Bakayoko hucheza kama box to box midfielder.
Eneo ambalo humtaka yeye kutimiza majukumu ya kukaba na kushambulia kwa pamoja, hutakiwa kurudi nyuma kukaba na kwenda mbele kushambulia.
Lakini kila anapokuwa anaenda kushambulia huwa anamakosa mengi na anapokuwa anarudi kukaba huwa anafanya makosa.
Makosa Anayoyafanya Wakati Wa Kukaba.
Covering, mara nyingi timu inapokuwa inakaba, moja ya wachezaji ambao huhusika kwa ajili ya kukaba katika eneo la nyuma ni Bakayoko.
Kuna wakati hajui kusimama sehemu sahihi ambayo itamsaidia kutimiza majukumu yake ya kukaba vizuri, mfano kuna wakati akiwa nyuma, unaweza kuta beki wa kati ametoka kwenda kumkaba mpinzani hivo huacha nafasi yake nyuma wazi, ambapo inahitajika mtu aje kuziba nafasi yake ( ku cover) , mazingira kama haya Bakayoko huwa anajikuta amesimama sehemu ambayo hatakiwi kuwepo na kushindwa kwenda kuziba (ku cover) nafasi ya beki aliyeondoka kwenda kumkaba mpinzani.
Tackles, moja ya kitu ambacho Bakayoko hakifanyi vizuri wakati wa kukaba ni kufanya tackling na hii ni kwa sababu ya aina yake ya uchezaji. Mara nyingi hukimbia nyuma ya mpinzani hivo anapojaribu kufanya tackling akitokea nyuma ya mpinzani hujikuta anafanya madhambi.
Makosa Anayoyafanya Wakati Wa Kushambulia.
Kushinda kukaa na mpira, mara nyingi anapokuwa anapewa pasi hujikuta hawezi kutuliza vizuri hali inayofanya kupoteza mipira virahisi, na kila anapopoteza mipira virahisi husababisha timu yake ipoteze umiliki wa mpira, na timu inapopoteza umiliki wa mpira inakuwa imevuruga mipango yake ya kushambulia. Kitu kikubwa ambacho huwa kigumu kwake hapa ni ule mpira wake wa kwanza anaoupokea kutoka kwa mchezaji mwenzake wa Chelsea, ambapo hushindwa kuhold vizuri na kujikuta amepokonywa mpira ule.
Kupiga pasi ambazo hazina macho. Bakayoko anawastani wa kupoteza pasi kuanzia 7-9 katika mchezo mmoja, na katika mechi iliyopita dhidi ya Watford kwa dakika 30 alizocheza alipoteza pasi 7. Kitu ambacho ni kibaya kwa mchezaji ambaye anacheza katika eneo la kiungo kwa sababu yeye ndiye anayetakiwa kuwa mchezaji ambaye ubunifu wa mashambulizi yanatokea kwake. Timu haiwezi kuwa na ubunifu wa kutengeneza mashambulizi kama kiungo wake wa kati anapiga pasi ambazo zinapotea mara nyingi.
Dhaifu la mwisho la Bakayoko katika jukumu la kushambulia ni umaliziaji hafifu.
Amekuwa anakosa utulivu anapotakiwa kufanya umaliziaji hali ambayo inamsababisha akose nafasi nyingi za ufungaji wa magoli na wakati mwingine amekuwa hapigi vizuri pasi za mwisho kwa sababu ya kukosa ƴutulivu. Mpaka sasa amecheza michezo 35 na akiwa amefunga magoli 3 na kutoa pasi 3 za mwisho, takwimu ambazo ni za chini ukilinganisha na eneo analocheza, takwimu ambazo zimemfanya azidiwe na Marcos Alonso na Cesar Azpilicueta ambao ni mabeki.
Marcos Alonso amecheza michezo 34 na kufunga magoli 7 na kutoa pasi 2 za mwisho, wakati Cesar Azpilicueta amefunga goli 2 na kutoa pasi 6 za mwisho.
Mara nyingi mashabiki humfurahia mchezaji anapofanya vizuri, hawana uvumilivu kipindi mchezaji anapokuwa anafanya vibaya. Hivo Bakayoko anatakiwa afanye jitihada kubwa kurudisha kiwango chake, msimu huu ni wa kwanza kwake katika ligi kuu ya England ana muda wa kuzoea zaidi na kufanya vizuri.