Makamo mwenyekiti wa Yanga Araphat Haji pamoja na viongozi wenzake wa Yanga wamefikisha mwaka mmoja wa kuiongoza Yanga tangu waingie madarakani mwaka jana.
Baada ya kukamilisha mwaka mmoja akiwa kiongozi wa Yanga mwenye mafanikio katika mwaka huo mmoja alisema “Wiki kama hii mwaka uliopita, wanachama wa Yanga walitumia haki yao ya kikatiba, waliniamini na kunichagua kuwa Makamu wa Rais wa klabu yetu. Julai 10, 2023 nimetimiza mwaka mmoja nikiwa Makamu wa Rais wa Yanga,” alisema na kuongeza
“Natumia fursa hii kuwashukuru wanachama, mashabiki na wapenzi wa Yanga kwa imani kubwa mliyonayo kwangu na uongozi mzima uliopo madarakani.”
Makamu huyo ambae ameshirikiana na Rais Hersi Said kuiongoza Yanga yenye mafanikio amewapa matumaini Wanachi huku akiahidi mambo mengi mazuri zaidi.
“Msimu uliopita (2022|23) ulikuwa ni msimu wetu wa kwanza madarakani, tumefanikiwa kushinda mataji yote tuliyoshiriki kwenye mashindano ya nyumbani lakini kwa upande wa mashindano ya kimataifa tumefika Fainali ya Kombe la Shirikisho na kumaliza katika nafasi ya pili.”
“Wananchi naomba muendelee kuniamini pamoja na uongozi mzima wa Yanga chini ya Rais wetu Hersi Said ili tuendelee kuipeleka klabu yetu kwenye mafanikio zaidi.
Ile ahadi yetu iliyobaki kwa timu zetu nyingine sasa wakati wake ndio umefika na tunakuja kuendeleza furaha zaidi. Msitishwe na wazee wa ‘Recycle Bin’ vyuma vinashuka muda si mrefu na ni vyuma kwelikweli na mshindo mmoja.”