Sambaza....

Uongozi wa klabu ya soka ya Arsenal umetoa ufafanuzi wa kwanini wameamua kumteua kocha Unai Emery kuchukua mikoba ya kocha Arsene Wenger ambaye ameondoka klabuni hapo msimu huu licha ya Mikel Arteta kupewa nafasi kubwa zaidi.

Stan Kroenke ambaye anamiliki hisa kubwa zaidi katika klabu hiyo yenye maskani yake jijini London amesema kocha Emery ameuthibitishia uma wa wanakandanda duniani kuwa ni mshindi wakati mtendaji mkuu Ivan Gazidis akisema kuwa utendaji kazi wa kocha huyo ndio uliwavutia zaidi.

“Unai amekuwa na rekodi nzuri katika maisha yake ya soka, ameweza kutengeneza vipaji vya wachezaji wengi chipukizi hapa Ulaya na wanacheza vizuri sana, aina yake ya uchezaji inafaa kwa klabu yetu, uwajibikaji wake na shauku ya mafanikio ndani na nje ya uwanja inamfanya kuwa mtu sahihi zaidi kwa kazi hii ili kutupeleka kwenye mafanikio” Gazidis amesema.

“Tulifanya upembuzi yakinifu na wa siri, tukiangalia maeneo mengi ikiwemo histori ya nyuma, data na uchambuzi wa video pamoja na kukutana ana kwa ana na wote waliopita katika mchuyo wa mwisho, wote walikuwa wazuri kwa nafasi hii lakini tumemchangua Unai kutupeleka pale ambapo tunapahitaji,” Gazidis ameeleza.

Unai ambaye ni kocha wa zamani wa Lorca Deportiva (2004-2006), Almería (2006-2008), Valencia (2008-2012), Spartak Moscow (2012), Sevilla (2013-2016), Paris Saint-Germain (2016-2018) ameteuliwa kuwa kocha mkuu wa Arsenal kuchukua mikoba ya Arsene Wenger.

Kwa wiki kadhaa sasa kocha Msaidizi wa Manchester City Mikel Arteta alikuwa akipewa nafasi kubwa ya kuchukua mikoba hiyo hadi kufikia kocha Pep Guardiola kutoa Baraka zake lakini meza imepinduka na ikielezwa kuwa uzoefu ndio silaha iliyomshinda dhidi ya Unai

Taarifa zinasema baada ya kushindwa katika mbio hizo sasa Arteta ataendelea na kazi yake katika klabu ya Manchester City licha ya tetesi kusema kuwa anaweza kupelekwa katika klabu ya New York City ya Marekeni baada ya kuwepo kwa taarifa za Patrick Viera kuomba kuondoka akihusishwa na vilabu vya Nice na Everton.

Sambaza....