UNCLE Mrisho Ngassa siku hizi anashinda mitandaoni kulalamika kuhusu madeni yake na Yanga. Analalamika sana mpaka anatia huruma.
Kupanga ni kuchagua. Siku nyingi tu uncle aliichagua njia hii. Haishangazi kuona leo hii, anatoa machozi ya damu peke yake. Hana wa kulia nae. Hana wa kumbembeleza. Analia mwenyewe.
Uncle alitakiwa kuondoka nyumbani miaka kumi iliyopita kwenda nje kuyakimbia malalamiko haya, lakini kwa makusudi kabisa alizikataa ofa nyingi zilizokwenda kwake na kuamua kuufurahia ufalme wake wa Jangwani.
Timu nyingi zilimtaka na kuamua kumtafuta hadi katika simu. Uncle kuona anapigiwa simu za kutakiwa aliamua hadi kuzima simu yenyewe asisumbuliwe.
Akaigeuza Yanga kama pepo yake ndogo na hakutaka kusikia jina la timu nyingine katika ngoma zake za masikio. Aliamini kila leo angeendelea kuwa uncle yule yule.
Inaonekana wakati ule aliona raha akikatisha mtaani jina lake likitamkwa mara nyingi na mashabiki, huku baadhi yao wakimuita na kumpa ofa na pesa ambazo hajazifanyia kazi. Hapa kulimfanya akashindwa kuifikiria kesho yake.
Ni hapa alipokosea uncle, leo hii anatuonyesha kuwa alijiandaa kushindwa, wacha ashindwe. Kama uncle angefikiria nje ya boksi zile ofa za wakati ule, leo hii angekuwa haongelei kuhusu madeni yake ya usajili na Yanga. Angekuwa ‘anapost’ magari yake tu kama anavyofanya Mbwana Samatta mtandaoni kwa sasa.
Kuna sehemu uncle hajafikiria vizuri, lakini hili hawezi kulikiri mbele yetu. Kibaya zaidi wale wote waliokuwa wanamzunguka wakati ule na kumpa ujeuri wa kumwambia azime simu ili asitafutwe na kwa sasa hawako tena pembeni yake. Yuko mwenyewe na majuto mengi kichwani. Hili hawezi kulikiri kwetu.
Mashabiki wa soka nchini hawajawahi kuwa na adui wa kudumu wala rafiki wa kudumu. Inategemea unawafanyia kitu gani katika muda gani. Siku zote wako hivi. Hawana unafiki.
Leo hii uncle sio mfalme tena Jangwani, ni mchezaji wa kawaida ambaye akicheza sawa na asipocheza sawa. Hivi sasa ni ngumu kuona kundi la mashabiki limesimama jukwaani likitaka uncle aingie akaikomboe timu ikiwa inahitaji matokeo. Wengi wameshayatoa macho kwake, hawaamini kama uncle ana maajabu miguuni mwake. Kwanza wanaona kitendo cha kuwa mchezaji wao mpaka leo ni kama wanamsaidia.
Uncle alijiandaa kuishi maisha haya. Wenzake wachache waliyakataa maisha haya mapema wakaondoka nchini, leo hii wanaporudi na kupiga picha katika viwanja vya ndege tunawaita mashujaa.
Inatia huruma mtu kama uncle kukaa mitandaoni kulalamika kuhusu pesa ambayo angekuwa nje angeingiza fedha nyingi zaidi ya hii anayoilalamika.
Uncle alitakiwa kuwa na fedha nyingi zaidi ya hizi alizonazo sasa kupitia miguu yake. Kibaya zaidi wale waliomshangaa alipozima simu wakati ule, leo hii ndiyo anawageukia kutaka huruma yao.
Inafikirisha sana. Kuna darasa wanalopaswa kulipata vijana wanaokuwa hivi sasa. Zaidi ni marafiki zangu wengi. Miaka kumi nyuma uncle alikuwa wa moto sana. Timu nyingi zilimfuata kumpa mikataba minono kumsaini, sio kumfanyia majaribio, lakini yote hakuyaona, aliamua kubaki Yanga. Leo hii Mapedeshee wamemkimbia na wamehamia kutembea na kina Molinga katika magari yao ya kifahari. Hawamtaki tena uncle.
Inatia huruma, baada ya miaka mingi uncle anaweza kukusanya kijiji cha wajukuu zake kuwaeleza hili, lakini hilo hawezi kutueleza sisi. Pole sana uncle!