Kuna vingi kwenye dunia hii huja kwa ajili ya kutuburudisha na kutufurahisha. Mwanadamu pekee huchagua sehemu ya yeye kuegemea ili kufurahi kutoka na kitu anachokipenda.
Ndiyo maana wengi hupenda kusema tunatofautiana. Huu ndiyo ukweli, tunatofautiana kabisa licha ya kuishi katika dunia moja.
Tunavuta pumzi sawa , tunamulikwa na mwanga sawa lakini mwisho wa siku tunatenganishwa na mstari mmoja wa matamanio.
Kila mmoja ana matamanio tofauti na kila mmoja anavitu ambavyo hutamani kuwa navyo ili afurahie akiwa kwenye dunia.
Na hapa ndipo utakapokuja kugundua kuwa dunia imebeba watu wa aina tofauti kabisa ambao huwezi kuwalazimisha wawe sawa kwa wakati mmoja.
Kwenye dunia hii ambayo Diamond Platinumz anatumika kama sehemu ya kutoa furaha kwa watu mbalimbali, ndiyo dunia hiyo hiyo ambayo Lebron James husimama kama mtengeneza furaha kwa wengine.
Yani tunatofautiana sana, tunapishana sana. Ndiyo maana mimi naweza nisiupende, hata kutouelewa kabisa mchezo wa Cricket lakini kuna watu hawawezi kula kipindi timu yao ya Cricket inaposhindwa.
Utamwambia nini mtu anayependa Tennis akiuelewa mpaka aje ashabikie mpira wa miguu ? Hapana shaka huwezi kumwambia kitu chochote na akakuelewa.
Ila unaweza ukafanya kitu kimoja bora ambacho kinaweza kumshawishi sana na yeye kufikiria kuupenda mpira wa miguu.
Kitu gani hicho ? Simpo tu, Fanya kumpeleka kwenye mechi ya mafundi. Mafundi ambao watashughulika kukarabati moyo wake mgumu.
Mafundi ambao wataonesha ufundi mkubwa uwanjani na kumfanya yeye mwenyewe abadilike taratibu na kuuweka mchezo wa mpira wa miguu kuwa moja ya mchezo anaoupenda duniani.
Unakumbuka enzi za kina Ronaldinho Gaucho? Mchezaji ambaye alikuwa amejaliwa kila aina ya sanaa katika miguu yake ambaye iliumbwa tofauti na MUNGU.
Mungu alitumia muda mwingi sana kutengeneza miguu ya Ronaldinho Gaucho, alitumia kila aina ya ufundi ili kumleta duniani binadamu aliyekuwa anaweza kuburudisha kupitia miguu yake.
Haimanishi MUNGU alikosea kuumba miguu ya wachezaji wengine. La Hasha,kazi ya MUNGU imekamilika ipasavyo ila kwa Ronaldinho Gaucho aliweka kitu cha ziada ambacho kwenye miguu mingine hakikuwepo.
Kitu gani hicho ? Sanaa! , aliweka sanaa ya kila aina kwenye miguu yake. Ungetaka nini kwenye miguu ya Ronaldinho Gaucho ukakosa ?
Kila ambacho ungetaka kilikuwepo. Kila aina ya muziki ulikuwepo katika miguu ya Ronaldinho Gaucho.
Hata kama unapenda gitaa, miguu yake ilikuwa inaweza kupiga kila aina ya gitaa na ukafurahia wewe mwenyewe.
Usiulize kuhusu kinanda, huyu ndiye mwanadamu pekee ambaye alikuwa fundi wa kinanda kupitia miguu yake peke yake.
Kwa kifupi kila aina ya sanaa ilikuwa katika miguu ya Gaucho , ndiyo maana aliweza kutengeneza tabasamu kubwa kwenye nyuso za walio wengi.
Ndiyo maana aliweza kuwashawishi wengi wapende mpira wa miguu. Kipindi cha Ronaldinho Gaucho hata mabinti wetu ambao ni nadra kupenda mpira wa miguu waliupenda ipasavyo.
Ndicho kipindi ambacho dunia ilikubali kuongea lugha moja. Leo hii kaondoka hatuko naye tena katika dunia yetu ya mpira wa miguu.
Jana wakati natazama mechi kati ya team Samatta na team Kiba kuna kitu nilikigundua, Ibrahim Ajib na Haruna Niyonzima ni watu wengine ambao wanaweza kuifanya dunia izungumze lugha moja kama wakicheza pamoja.
Walikuwa wanaonesha burudani ambayo binadamu yeyote yule ambaye hapendi mpira wa miguu huwezi kutumia nguvu nyingi kumshawishi zaidi ya kumpeleka uwanjani na kumuonesha Ibrahim Ajib na Haruna Niyonzima wakicheza pamoja.