Sambaza....

Kocha wa Liverpool Jurgen Klopp amesema haoni kabisa kama mshambuliaji wake raia wa Misri Mohamed Salah anasumbuliwa na tatizo la msongo wa mawazo kutokana na kushindwa kuzitingisha nyavu katika michezo nane iliyopita.

Salah ambaye msimu uliopita alifunga mabao 44 katika mashindano yote, msimu huu umekuwa mgumu kwake akifunga mabao 20 pekee na mara ya mwisho kufunga ilikuwa Februari 9 mwaka huu, licha ya kuhusika kwenye ushindi dhidi ya Tottenham Jumapili iliyopita ambapo alisababisha bao la kujifunga la Toby Alderweireld katika dakika za majeruhi.

“Lilikuwa ni bao la kujifunga lakini ni kichwa cha Salah ndiyo kililazimisha hali ile, na yeye alihisi kama goli lilikuwa ni lake, maisha yake ya soka bado hayajaisha, ni kama kusema hivi kaweza kufunga mabao 20 msimu huu, hivyo kumfanya kwa misimu miwili kufunga zaidi ya mabao 60, Wow! hicho sio kitu kibaya.” Klopp amesema.

“Kama ungekuwa unamtegemea mfungaji mmoja labda lingekuwa tatizo, lakini msimu huu hatutegemei mabao ya Salah pekee, lakini yupo katika hali nzuri zaidi ukilinganisha na wachezaji wengine kwenye timu, yeye ni tishio, ametusaidia sana, na yupo katika hali nzuri kwa kukubaliana na kila hali ambayo ipo naye kwa sasa,” Klopp ameongeza.

Liverpool ambao wanakalia katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi kuu England kwa alama 79 watakuwa na mchezo mwingine mgumu dhidi ya Southampton siku Ijumaa na ushindi utawarudisha tena kileleni dhidi ya Manchester City.

Sambaza....