Kocha mkuu wa Biashara United ya mkoani Mara Hitimana Thiery ameitaja safu yake ya ushambuliaji kuwa ndio chanzo cha kupoteza katika mchezo wa ligi dhidi ya Stand United, kwani mbali na kukosa nafasi nyingi za wazi lakini pia waliwakosa wachezaji tegemeo katika eneo hilo.
Akizungumza na mtandao huu, Hitimana amesema katika mchezo huo ambao walipoteza kwa bao 1-0 waliwakosa wachezaji muhimu kama Uhuru Suleiman na Astin Amos ambao wote hawakuwa katika mipango yake kutokana na sababu mbalimbali.
“Tatizo hasa lilikuwa katika safu ya ushambuliaji, unajua sisi tunavijana wadogo ambao waliipandisha timu wale ambao tulikuwa tunawatumainia watatusaidia kama Uhuru Suleiman walipata tatizo la msiba sasa kukosa wachezaji wawili hadi watatu ni kazi kupata ushindi,” amesema.
Mbali na hilo Hitimana amesema kucheza michezo mitatu mfululizo ugenini nalo limechangia pa kubwa kupata matokeo hayo ambayo kimsingi sio mazuri kwani wameshinda mchezo mmoja tu wakiruhusu kufungwa michezo miwili mfululizo.
“Sisi ni timu ndogo, ndio kwanza tumepata ligi, unajua kuanzia mechi tatu ugenini nayo sio kitu rahisi, halafu unakuja kukutana na timu ambayo ilikuwa hapa hapa inawasubiri haiwezi kuwa rahisi,” Ameongeza.
Mpaka sasa Biashara United wamecheza michezo mitatu na kufanikiwa kushinda mchezo mmoja dhidi ya Singida United kabla ya kupoteza dhidi ya Coastal Union na Stand United, na mchezo ujao watakuwa katika uwanja wao wa nyumbani wa Karume mjini Musoma kucheza na Kagera Sugar.