Sambaza....

Ushindi wa Timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) dhidi ya Uganda kwenye mchezo wa kuwania nafasi ya kufuzu kwenye fainali za Mataifa Afrika (AFCON) umeifaidisha si tu kufuzu bali hata kupanda kwenye nafasi za ubora wa soka Ulimwenguni.

Viwango hivyo vinavyotolewa na shirikisho la Kandanda Ulimwenguni (FIFA) inaonesha kuwa Tanzania imepanda nafasi sita kwa mwezi wa tatu kutoka nafasi ya 137 hadi nafasi ya 131 kwa kukusanya alama 1105 kutoka alama 1087 za mwezi uliopita.

Vinara kwa upande wa nchi mwanachama wa shirikisho la soka kwa vyama vya ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) Uganda wao wameporomoka kwa nafasi mbili kutoka nafasi ya 77 hadi nafasi ya 79 kwa mwezi huu.

Nchi nyingine za CECAFA ikiwemo Kenya imeporomoka kwa nafasi mbili sasa inashika nafasi ya 108, Burundi wanashika nafasi ya 136 wakipanda kwa nafasi mbili, Rwanda wakishika nafasi ya 138 wakiporomoka kwa nafasi mbili huku Sudan Kusini wao wakishika nafasi ya 167.

Kwa upande wa Afrika Senegal inashika usukani huku kwa dunia ikishika nafasi ya 23, ikifuatiwa na Tunisia (28), Nigeria (42), Morocco (45) na tano bora inafungwa na Congo DR (46).

Kwa upande wa dunia, England imeingia kwenye nne Bora kwa kushika nafasi ya nne huku nafasi tatu bora za juu zikiwa hazina mabadiliko yoyote kwa Ubeligiji kuongoza viwango vya mwezi huu wakifuatiwa na bingwa wa kombe la dunia la mwaka jana Ufaransa na tatu bora inafungwa na Brazil, huku nafasi ya tano ikishikiliwa na Croatia.

Sambaza....