Sambaza....

GOLI la kichwa la mshambulizi, Patrick Henry dakika 11 kabla ya kumalizika kwa mchezo limeipa Uganda ´Korongo´ tiketi ya kufuzu kwa mara ya pili mfululizo fainali za Mataifa ya Afrika.

Katika mchezo mgumu wa kundi L jioni ya Leo katika uwanja wa Namboole, Kampala wenyeji walionekana kama wangepoteza, kabla ya mlinzi wa kushoto, Godfrey Walusimbi kufanya ´uchawi´ wake alipopandisha timu haraka na kupiga ´krosi-pasi´ maridadi iliyotokewa haraka pia na Henry ambaye alifunga kwa kichwa kikali cha kupara mpira uliokuwa na nguvu kutoka kwa Walusimbi.

Golikipa, Dennis Onyango ambaye pia ni nahodha wa Korongo alimaliza mechi akiwa na maumivu yanayosadikiwa kuwa ya nyonga, lakini aliendelea kuzuia mashambulizi kadhaa ya Cape Verde na robo saa yake ya mwisho aliyocheza na maumivu ameendelea kuimarisha rekodi yake ya kutoruhusu goli,.

Na baada ya Itumelenge Khune wa Afrika Kusini kuruhusu goli vs Nigeria, Onyango anabaki kuwa golikipa pekee asiyeruhusu nyavu zake kufikiwa na mpira katika magolikipa wote walioziwakilisha nchi zao katika kampeni hii inayoelekea mwisho kuwania tiketi ya kwenda Cameroon katika fainali za Juni mwakani.

Msimamo wa kundi

NIDHAMU

Uganda wameendelea kubebwa na nidhamu yao ya mchezo. Wametawala kundi, wamekusanya alama 13 katika michezo mitano. Walitumia vizuri uzoefu wa Onyango golini, Jjuuko Murshid , Walusimbi, Hassan Waswa katika ngome na Emmanuel Okwi katika mashambulizi.

Wachezaji hao wazoefu (kutoa Okwi) walikuwepo wakati Uganda walipofuzu kwa mara ya kwanza CAN2017 baada ya kusubiri tangu mwaka 1978.

Hawa wamekuwa nguzo kubwa na taswira ya uzoefu katika timu. Faroq Miya amefunga magoli matatu katika kampeni hii ya kwenda Cameroon 2019, Henry ambaye alianza mahala pa Okwi aliyekuwa akitumikia adhabu ya kutocheza kutokana na kuwa na kadi mbili za njano, mlinzi wa kulia, Nicolaus Wadada ni mfano wa namna Uganda isivyo na hofu ya kuamini vipaji vipya, lakini msingi wao wa timu unajengwa vizuri tangu wakati wa kina Andy Mwesigwa, David Obua, Tonny Maweje na Onyango ambaye bila shaka atawaachia Jjuuko na Walusimbi mara baada ya fainali za mwakani.

Uganda wamelindwa na nidhamu yao kila wanapocheza Namboole, na tayari Mataifa kama Misri, Cameroon, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Tunisia, Senegal, Mali, yanajua hawawezi kupata pointi tatu katika uwanja huo.

Katika kampeni ya kwenda Cameroon mwakani, Korongo wamezifunga ´nyumbani na ugenini´ Cape Verde na Lesotho, Tanzania wakapata suluhu. Wamekusanya pointi saba kati ya tisa walizopaswa kuzipata, wakaenda ugenini kwa nidhamu zaidi na kukusanya alama sita kati ya sita walizojaribu kuzipigania.

Nidhamu yao katika ujenzi na undelezaji wa kikosi, nidhamu yao katika uwanja wa nyumbani na jitihada zao uwanjani wanapocheza ugenini pia kumewabeba katika malengo yao. Wana mipango mizuri ya kuvumbua na kuendeleza vipaji vyao kila vinapoibuka.

WATAKUJA DAR KUWAFUNDISHA…

Baada ya ushindi wa Uganda vs Cape Verde jioni ya Leo, Tanzania inaweza kufuzu kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1980 endapo wataifunga Lesotho ugenini kesho Jumapili.

Watanzania wengi wanasema ´Uganda katumalizia kazi´. Siamini hivyo- Korongo wamejibeba wenyewe na ili kupata wa kuungana nao kutoka kundi L, ni lazima Lesotho, Tanzania na Cape Verde wajibebe wenyewe.

Stars itachapwa kesho, na sitashangaa Uganda akimaliza tarajio la ghafla la Watanzania jijini Dar es Salaam. Lesotho ana nafasi kubwa kwa sasa ya kuungana na Uganda- kama si wao Cape Verde. Tanzania wajifunze kwanza kutoka kwa Uganda kabla hawajaja kuwafunza.

Sambaza....