Sir Alex Ferguson bila shaka ni miongoni mwa makocha waliokuwa maarufu sana duniani na hadi leo umaarufu wake bado unaendelea. Ferguson alishawahi kuhojiwa na mtandao wa The SoccerStore juu ya sifa za kocha bora.
Bila kukupesa macho Mzee Furguson alijibu kuwa, Kocha bora ana sifa kuu 7:
1. kujijua mwenyewe ni aina gani ya kocha, ujijue udhaifu wako na ubora wako
2. Uwe mvumilivu na moyo wa subira
3. Uwe kiongozi
4. Uwe vizuri katika mawasiliano (communication skills)
5.muda wote uwe na mtazamo chanya
6. Uwe na moyo wa dhati wa kufanya kazi yako
7. Uwe mzuri wa kuchunguza vitu na mwisho kabisa uwe na uwezo wa kuvuta taswira chanya juu ya timu yako.
Ukiachana na haya ya Ferguson, pia ukiachana na Siasa za Soka la bongo, leo acha tuangazie udhaifu wa aliyekuwa kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera kiufundi.
Hapa tutaangalia jinsi Yanga ilivyokuwa ikicheza, matumizi ya Wachezaji, Maeneo gani muhimu yalikuwa ndio tegemezi kwake, Wachezaji muhimu katika mifumo yake na mwisho tutagusia makosa katika maandalizi ya mchezo mmojammoja kutokana na mahitaji yake.
Yanga ya Msimu uliopita.
Msimu uliopita na msimu huu mambo yamekuwa tofauti sana kwa Yanga kuanzia kiuchumi na hata aina ya wachezaji na uchezaji. Lakini kwa kuwa hapa tutamuangazia Zahera uwanjani acha kwanza nianze na kikosi cha msimu uliopita kisha tuangalia ni wapi Msimu huu kumekuwa na mabadiliko kiuchezaji.
Golini muweke Klaus Kindoki, Shavu la kulia mpe Paul Godfrey, kushoto Gadiel Michael, Mabeki wa kati Andrew Vicent Dante na Kelvin Yondani. Katikati Feisal Salumu, Papy Tshishimbi, Mrisho Ngassa, Mohammed Banka na Ibrahimu Ajibu, Mbele yupo Heritier Makambo.
Hapa walikuwa wakicheza mfumo wa 4-4-2 timu inapokuwa katika presha ya kawaida, Ajibu aliungana na Makambo kama Second Striker, huku Tshishimbi na Banka wakicheza juu kidogo ya Feisal Salumu, huku muda mwingi Tshishimbi akionekana kucheza eneo la chini, la kati na la juu, Katika mfumo huu walimuacha Ngasa kama winga asilia, mwenye uwezo wa kuongeza presha kwa beki wa kushoto wa timu pinzani.
Pia walitumia mfumo wa 4-3-3 timu inaposhambulia. Mfumo huu ulifanya vizuri pale Zahera alipoingia na washambuliaji wawili, yaani Amis Tambwe na Makambo ambao waliungana na Ajibu kuunda idadi ya washambuliaji watatu timu inaposhambulia.
Lakini pia hata bila ya kuanza kwa Tambwe, Tshishimbi aliungana na Ajibu na Makambo kuweka idadi ya wachezaji watatu wa yanga katika eneo la mpinzani timu inaposhambulia .
Mwisho kabisa walikuwa wakibadilika na kucheza 4-5-1 timu inaposhambuliwa. Hapa Ajibu alishuka chini kuungana na Tshishimbi, Banka, Feisal na Ngassa kuzuia mashambulizi na kumuacha Makambo pekee yake kama mshambuliaji wa mwisho kwa ajili ya kufanikisha mashambuli ya kushtukiza.
Msimu uliopita Yanga ilikuwa ikishambulia kupitia pembeni na katikati. Pembeni iliwatumia mabeki wake, Paulo Godfrey Boxer ambaye ni mzuri kukimbia na mpira, kasi yake ilikuwa ni nzuri na hata krosi zake nyingi zilikuwa na macho.
Tambwe na Makaambo waliiitumia vizuri Mipira ya Paulo na hata kufunga magoli ya vichwa. Pia walikuwa Gadiel Michael ambaye kiukweli alikuwa beki kisiki. Uzuri wa Gadiel ni uwezo wa kupita pembeni na kupiga mashuti langoni na hata kufunga, mfano ni goli alilofunga dhidi ya Azam.
Gadiel na Paulo waliipa uhakika Yanga kupata ushindi kwa wao kutengeneza krosi zilizowafikia washambuliaji wa kati na kufunga.
Yanga pia ilishambulia kupitia katikati, hapo Ibrahimu Ajibu, Tshishimbi na Feisal walionekana kuwa wazuri zaidi kwa kupiga pasi Mpenyezo na hata kushuti golini na kufunga magoli. Feitoto ni miongoni mwa wachezaji waliofanya vizuri zaidi msimu uliopita kwa kushambulia kupitia katikati na kupiga mashuti Mwana Ukome yaliyozaa mabao.
Ukiiangalia Yanga ya msimu uliopita ilikuwa imekamilika kwa maana ya ‘BALANCE’ Kwanza ilikuwa na mabeki wa pembeni wanaopiga Krosi na Washambuliaji wazuri kwa vichwa na mipira ya krosi. Pili Mpangilio wa mabeki ulikuwa ni wa kimkakati, Yaani Gadiel Akipanda, Paulo alilazimika kukaa mstari sawa na mabeki wa kati, ili kuweka uwiano sawa wa urefu kutoka nafasi ya beki wa kulia hadi kushoto.
Kwa upande wa viungo walicheza kwa kubadilishana majukumu kiutendaji yaani ALTERNATING. Viungo wa kati Tshishimbi, Feisal na Banka walikuwa na mawasiliano yaliyokomaa kwa maana Tshishimbi akipanda, Feitoto alihakikisha anabaki chini kama kiungo wa ulinzi, vivyo hivyo kwa Feitoto akipanda.
Hii ilisaidia Yanga kukaba kwa mpangilio na kusaidia kuipora mipira kirahisi na hata kuzuia pasi mpenyezo. Yaani Feisal akienda kukabia juu aliungana na mmoja kati ya Banka au Thishimbi huku mwingine akibaki chini kama kiungo wa ulinzi karibu kabisa na Mabeki wa kati na wakati mwingine kuziba eneo lilioachwa na Beki wa pembeni alipoenda kushambulia.
Kwa upande wa Safu ya ushambuliaji, Yanga iliongozwa na Heritier Makambo ambaye kwa kiasi kikubwa aliimudu nafasi hiyo. Zahera alimuanzisha pekee yake mbele katika mechi nyingi lakini ni chache alimuanzisha na Tambwe.
Makambo alionekana hatari zaidi katika mfumo wa 4-5-1 kutokana na staili yake ya kiuchezaji, Sifa zake na aina wachezaji wanaomzunguuka. Makambo alikuwa na kasi, uwezo wa kupiga vyenga, matumizi mazuri ya vichwa, kushuti eneo lolote, kujiweka katika maeneo ya hatari na kujua timu inahitaji nini na yeye afanye nini ili kuwahadaa mabeki.
Alionekana kama Straika katika kipindi cha kushambulia kwa kushtukiza lakini muda mwingi Makambo alijificha visogoni mwa mabeki, hii ilikuwa ni ngumu kwa wao kumkaba na kufanya kupiga vichwa akiwa huru na hata kukimbia na mpira katika maeneo ya wazi na kufunga mabao.
Yanga pia ilikuwa na Ajibu ambaye alikuwa akiibadili mipira ya faulo kuwa magoli au nafasi za magoli. Hii inamaanisha kuwa Yanga ilikuwa na njia nyingi za kupata matokeo.
Hadi kufikia hapa bila shaka utakuwa umemuelewa Zahera wa Msimu uliopita, Zahera ambaye aliisaidia Yanga nafasi ya pili na kuwaacha wengi midomo wazi.
Timu haikucheza mpira wa kuvutia sana lakini iliweza kupata ushindi, japo kwa shida lakini ushindi ni Ushindi. Ushindi huu ulichochewa sana na aina ya wachezaji waliopo kwani walijitoa sana kuhakikisha wanafanya vizuri licha ya kuwa na changamoto nyingi za kiuchumi.
Tuachane na msimu uliopita acha tujikite katika msimu huu, msimu ambao ulikuwa ni wa pili kwa Zahera na ndio ulisababisha atimuliwe.
Msimu huu una vitu vingi ambavyo kwavyo vimechangia kubadili mbinu za mchezo. Yanga imewapoteza baadhi ya wachezaji katika dirisha kubwa la usajili lakini pia, imeingiza wengine katika nafasi mbalimbali.
Yanga iliwapoteza wachezaji muhimu kama Ajibu, Abdallah Shaibu, Beno Kakolanya ,Gadiel Michael na Herithier Makambo lakini pia iliachana na Amis Tambwe, Kamusoko, Buswita na wengine kibao ambao kwa namna moja au nyingine walikuwa msaada kwa timu katika nyakati tofauti tofauti.
Zahera alijitahidi kusajili wachezaji wapya katika maeneo mbalimbali. Alisajili zaidi ya wachezaji 13, Wamo viungo kama Patrick Sibomana, Mapinduzi Balama na Abdulaziz Makame, Washambuliaji kama Maybin Kalengo, Sadney Khoetage, David Molinga na Juma Balinya, lakini pia alihakikisha anasuka ukuta kwa kumsajili Lamine Moro, Ally Ally,Mustapha Selemani, Muharami Issa MARCELO, na Ally Mtoni Sonso. Lakini pia langoni aliongeza magolikipa wawili, Metacha Mnata na Farouk Shikalo.
Fikiria kikosi kama hiki, Golini, Metacha Mnata, shavu la kulia, Paulo Godfrey, la kushoto Ally Mtoni, Katikati ni Yondani na Lamine. Viungo ni Abdulaziz Makame, Feisal Salumu, Patrick Sibomana na Mrisho Ngasa huku washambuliaji wakiwa ni Papy TShishimbi kama ‘Inside 10’ na Sadney kama Standing striker.
Acha tuangalie kiujumla kuanzia mechi ya kwanza klabu bingwa Afrika dhidi ya Township Rollers mechi ya awali hadi Shirikisho dhidi ya Pyramids FC.
Kumekuwa na mabadiliko mengi katika kikosi, hii ni katika harakati za kocha kutafuta muunganiko wa wachezaji. Yanga ilionekana kukosa muunganiko katika eneo la kati, huku timu ikishindwa kutengeneza nafasi nyingi za magoli na hata hizo chache zinazotengenezwa zilishindwa kutumiwa.
Katika kikosi hiki Zahera alijaribu kubadili mfumo na staili ya uchezaji tofauti na msimu uliopita. Yanga ya msimu huu ilitumia viungo wengi. Zahera aliamini kuwa magoli yanaweza kupatikana kwa kuwaanzisha viungo watano na mshambulaiji mmoja.
Kiufupi mashambulizi ya Yanga yalijikita kupitia katikati ya kiwanja. Mfano katika mechi dhidi ya Zesco United, Zahera alianza na Banka, Feitoto, Makame, Tshishimbi na Sibomana. Hii ilimaanisha kuwa Yanga iliingia na winga mmoja ambaye Kimuonekano angeshambulia kupitia pembeni.
Yanga ilishambulia kupitia katikati zaidi huku Sibomana akishuka chini zaidi muda mwingi kutimiza majukumu ya kiulinzi kwa kushirikiana na Ally Sonso au Mapinduzi balama.
Tofauti na Yanga ya msimu uliopita, Yanga hii iliamini katika kumiliki dimba na mpira kiujumla, kisha kutafuta nafasi za magoli. Zahera aliamini kuwa Sadney pekee kama mshambuliaji anaweza kuipa Yanga ushindi.
Zahera akiwaanzisha Sadney na Balinya kwa pamoja, mmoja lazima acheze kama winga na sio mshambuliaji. Mfano katika mechi dhidi ya Ruvu shooting , Molinga alibaki kuwa kama Mshambuliaji wa mwisho huku Sadney na balinya wakitokea pembeni kama mawinga.
Pia katika mechi dhidi ya Zesco United Maybin Kalengo aliingia kuchukua nafasi ya Sadney licha ya timu kuwa nyuma lakini Zahera anaonekana kuamini mfumo wa mshambuliaji mmoja.
Hili pia limejidhihirisha katika mechi dhidi ya Pyramids ambapo, Zahera alianza na Sadney pekee kama mshambuliaji wa mwisho huku Feitoto, Makame, Balama, Tshishimbi na Ngassa wakiwa eneo la kati.
Kimaandishi Yanga walicheza mfumo wa 4-4-2 kwa maana Tshishimbi alitakiwa aungane na Sadney lakini uwanjani walicheza 4-5-1 kwa Maana Tshishmbi hakuungana na Sadney mapema timu iliposhambulia, matokeo yake ni Sadney kukabwa kirahisi na kukosa msaada.
Yanga pia ilikosa huduma ya Paulo Godfrey ambaye angesaidia kushambulia kupitia pembeni na kuongeza idadi ya nafasi za kuandika magoli. Pia hadi leo Yanga imemkosa mrithi sahihi wa Gadiel Michael kwa upande wa kushoto. Mabeki wa pembeni waliopo kwa sasa hawashambulii, hapa nazungumzia Sonso, na hata Juma Abdul kwa sasa hana ubora wa kutengeneza nafasi za goli.
Hii inamaanisha kuwa njia pekee ya Yanga kupata ushindi na kutengeneza nafasi ni kwa kupitia katikati na mipira ya kutenga kama faulo na kona pekee. Hii ndio sababu ya Yanga kushindwa kutengeneza nafasi nyingi za
Niandikie hapo chini, unadhani kuondoka kwa Zahera kutaifanya Yanga kuongeza makali yake, ikiwa aina ya wachezaji waliopo wamesajiliwa na yeye?