Sambaza....

Nimeitazama timu ya Simba katika michezo yake takribani yote, zikiwemo zile mechi za ligi alizoshinda kwa ushindi mkubwa na zile za ushindi mdogo, sare, kufungwa na mechi za kirafiki.

Simba imekuwa na uimara kwa baadhi ya maeneo na udhaifu kwa baadhi ya maeneo pia, nikianza na udhaifu ambao kwa kiasi kikubwa ndio utakao waangusha Simba mbele ya Mbabane Swallows ni maeneo yafuatayo.

Golikipa.

Aishi Salum Manula ndiye golikipa anayeaminiwa zaidi katika kikosi cha Msimbazi, bila shaka ndiye atakayekuwa mlinzi wa goli katika mechi ya marejeano lakini naye anaudhaifu wake.

Kutema mipira karibu na maadui. Katika falsafa za kulinda goli, makocha wa makipa wanaamini kuwa, golikipa kazi yake si kudaka mipira bali ni kuiokoa isiingie golini lakini Manula amekuwa na udhaifu huo kwa mechi nyingi ikiwemo ile ya Taifa Stars dhidi ya Lesotho, kosa hilo lilizaa goli, pia katika mechi dhidi ya Uganda na hata katika mechi za ligi.

Bila shaka kama washambuliaji wa Mbabane watakuwa haraka kufika karibu na Manula baada ya kupiga shuti huenda wakawashangaza Watanzania.

Mashuti ya kushitukiza na ya mbali.  Kwa lugha nyepesi unaweza sema Manula huwa hawi mchezoni “game concentration”. Mchezo dhidi ya Mbabane swallows alipigiwa bunduki kisha akashindwa kuiokoa, dhidi ya Mbao, Manula alionesha udhaifu mkubwa katika kufuata mashuti ya mbali na yenye uzito wa haja. Endapo Mbabane watashambulia kwa kasi na kupiga mashuti hata nje ya 18, Simba lazima walale.

Eneo la ulinzi.

Eneo hili huundwa na golikipa pamoja na mabeki, Simba mara  nyingi hutumia mfumo wa 4-4-2 na 4-3-3, maana yake hucheza na mabeki wanne. Ukiitazama beki ya Simba unaiona ni beki ambayo haina muunganiko mkubwa, hasa kwa mabeki wa kati, Erasto Nyoni na Pascal Wawa. Mwanzoni mwa ligi walionekana kuwa na muunganiko mzuri lakini kukaa nje kwa Nyoni na kuingia kwa Juuko Murshid kikosini kunaufanya muunganiko wa Nyoni na Wawa upotee.

Mechi ya kwanza dhidi ya Mbabane, safu ya ulinzi ya Simba ilionekana kukosa muunganiko  na kuwafanya washambuliaji wa Mbabane kupata nafasi ya kumsabahi Manula.

Kwa upande wa Nyoni, amekuwa akishindwa kuokoa mipira ya vichwa, mipira yake huwa inaishia karibu na hata kumkuta adui, ana papara, si beki mzuri wa kuanzisha mashambulizi, itakuwa ni faida kubwa endapo Nyoni atacheza shavu la kulia na wala si beki wa kati japo uzoefu utambeba.

Pasco Wawa, amekuwa ni beki mwenye  sifa zinazostahili kuwa beki bora kwa sasa, japo hakuna kizuri kisicho na udhaifu. Wawa ni mzito hasa kwa mipira mpenyezo, na hata akikutana na mchezaji machachari “ one against one” Wawa huwa anakosa mbinu mbadala za kumzuia zaidi ya kufanya rafu mbaya, kwahiyo ni mwepesi kupitika katika mazingira hayo.

Pengo la Shomari Kapombe. Pengo la beki kisiki wa shavu la kulia bado halijazibika, anayecheza nafasi hiyo bado hajaonesha thamani sawa na kapombe akiwa uwanjani. Nicolas Gyan alicheza vizuri katika mechi ya kwanza dhidi ya Mbabane  lakini ana tatizo la kukosa muendelezo. Kiasili Gyan ni mshambuliaji na si beki hivyo hujikuta muda wote anashambulia akisahau jukumu lake mama la kulinda, hii ni tofauti na kapombe ambaye anaweza kukupa vyote kwa wakati mmoja.

Eneo la kiungo.

Hili ndio eneo nyeti kwa timu ya Simba, funguo za ushindi kwa klabu hii katika mechi zote ziko katika eneo hili. Mbabane Swallows wanaonekana kuwa wazuri katika eneo hili, hivyo endapo Aussems atafanya uteuzi mbovu wa kikosi chake hasa katika eneo hilo atawaruhusu Mbabane kumiliki mpira, na kutengeneza nafasi nyingi za magoli.

Katika mechi ya kwanza, eneo la kiungo la Simba chini ya James Kotei na Jonas Mkude lilionekana kufunika vuguvugu za viungo wa Mbabane japo ilikuwa ni kwa vipindi. Clatus Chama ambaye alikuwa muhimili mkubwa aliachwa kucheza huru akitokea kulia huku Emmanuel Okwi akitokea kushoto, Simba walifanikiwa.

Mechi hii ya marudiano, inatakiwa mwalimu abadili mbinu, hasa kuanza na mfumo wa viungo wawili wakabaji, yaani Kotei na Mkude wawe viungo wa chini (holding Midfielders) huku Chama akicheza kama namba nane, akisaidiwa na Okwi wakati huo John Boko na Meddie Kagere wakibaki kuwa washambuliaji wa mwisho. Lengo la mfumo huu ni kuhakikisha Simba inakuwa salama inapokuwa na mpira na hata ikiwa  haina.

Mwisho kabisa naweza kusema kuwa, mpira ni mchezo wa makosa, timu ikifanya makosa inaweza kuadhibiwa hapo hapo. Simba itashinda endapo tu kama wachezaji wote watakuwa katika kiwango kinachotarajiwa  na kilichozoeleka.

Mfano, kama wachezaji wote wa Simba wakicheza kama alivyocheza Okwi katika mechi ya kwanza bila shaka magoli yatafungwa zaidi ya matatu na hatimaye Simba itatolewa.

Nikiutizama mchezo huu nakumbuka klabu bingwa ulaya msimu wa 2016/17, PSG iliwalaza  miamba ya Hispania Barcelona 4-0 lakini pale Nou Camp PSG walilala kwa goli 6-1 ni nani alidhani kama PSG wangetolewa, Msemaji wa Ruvu Shooting, Masau Bwire huwa anasema “Mpira Unadunda”.

Namalizia kwa kusema , sisi kama watanzania tuziombee timu hizi mbili (Simba na Mtibwa) zinazoiwakilisha nchi zifanikiwe na kusonga mbele katika michuano hii kwa tija ya taifa kwa ujumla.

 

 

Sambaza....