Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29, kwa mara ya mwisho alionekana katika mchezo wa ligi ya England mwishoni mwa juma lililopita dhidi ya Chelsea akiingia kama mchezaji wa akiba.
Meneja wa United Jose Mourinho amesema Sanchez hana utimamu wa mwili (hayupo FIT), na ameona ni bora kumpumzisha katika mpambano wa leo, ambao unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani kote.
Mourinho pia amethibitisha kuwa na uhakika wa kumtumia beki wa pembeni Antonio Valencia, kwa mara ya kwanza baada ya kumkosa kwa muda wa majuma matatu, kufuatia kufanyiwa upasuaji mdogo wa mdomo.
Akizungumzia uwezekano wa kurejea kwa Valencia, meneja wa United Jose Mourinho amesema, “Alikua mgonjwa, alifanyiwa upasuaji mdogo kwenye mdomo, kuna uhakika wa kumtumia katika mchezo wetu dhidi ya Juventus, Sikumchezesha katika michezo kadhaa tangu Oktoba 02, kwa sababu alihitaji muda wa kupumzika na kujiuguza.”
Kwa upande wa mabingwa wa soka nchini Italia Juventus FC, wanachagizwa na kurejea kwa mshambuliaji wao hatari Cristiano Ronaldo, baada ya kumaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyooneshwa wakati wa mchezo wa mzunguuko wa kwanza hatua ya makundi dhidi ya Valencia, Septemba 19.
Ronaldo anatarajiwa kucheza dhidi ya Mannchester United akiwa na klabu ya Juventus, kwa mara ya kwanza tangu alipoihama Real Madrid mwishoni mwa msimu uliopita.
Kwa mara ya mwisho mshambuliaji huyo aliyeitumikia United kuanzia mwaka 2003-2009, alicheza kwenye uwanja wa Old Trafford akiwa na klabu ya Real Madrid mwaka 2013.
Wakati Ronaldo akitarajiwa kurejea kikosini hii leo, Juventus huenda wakawakosa mshambuliaji kutoka nchini Croatia Mario Mandzukic, kiungo wa zamani wa Liverpool Emre Can pamoja na Sami Khedira.