Leo Yanga walianza na mfumo wa 4-3-3 baadaye walibadirika na kuanza kucheza 4-4-2 na Njombe mji wakicheza mfumo wa 4-4-2.
Kwa kipindi cha kwanza Njombe mji walicheza vizuri wakati wakiwa na mpira kuanzia eneo la nyuma mpaka katika eneo la katikati.
Walipokuwa na mpira waliweza kusogea mpaka eneo la karibu na kumi na nane ya Yanga ila walikosa uwezo wa kupiga pasi ambazo zingevuka ukuta wa Yanga na wao kupata goli.
Kelvin Yondan alifanikiwa kwa kiasi kikubwa kuwa kiongozi bora wa Said Makapu. Pamoja na kwamba Said Makapu ni mchezaji wa eneo la kiungo cha kuzuia kiasili lakini alifanikiwa kuwa mtulivu katika eneo la beki wa kati.
Yeye pamoja na Kelvin ndiyo walikuwa wanaanzisha mashambulizi hasa hasa kipindi cha kwanza.
Mfano, katika kipindi cha kwanza Yanga walikuwa wamepanga kutumia mipira mirefu ya moja kwa moja ( direct football) kwa kina Emmanuel Martin, Obrey Chirwa na Pius Buswita ambaye dakika nyingi za kipindi cha kwanza alicheza kama mshambuliaji wa kati huku pembeni kulia alikuwepo Chirwa na Emmanuel Martin akawa anacheza pembeni kushoto.
Pamoja na kucheza katika eneo la mshambuliaji wa kati katika dakika nyingi za kipindi cha kwanza , Pius Buswita alikosa jicho la mshambuliaji wa kati. Alitengenezewa nafasi nyingi kipindi cha kwanza kwa kutumia mipira mirefu na kina Kelvin Yondan lakini alikosa utulivu wa kufanya maamuzi ya mipira aliyotengenezewa.
Makka alikuwa anatimiza majukumu yake vizuri katika kiungo cha kati , hali ambayo ilimpa nafasi nzuri Papy Kabamba kutimiza majukumu yake vizuri kama Box to box , ambapo alikuwa anapamba kushambulia na kurudi kukaba, Raphael Daud pekee ndiye ambaye alikuwa mzito kufanya maamuzi akiwa na mpira hata wakati ambao hakuwa na mpira.
Kutoka kwa Raphael Daudi na kuingia kwa Juma Mahadhi katika kipindi cha pili kiliifanya Yanga ibadili mfumo kutoka mfumo wa 4-3-3 na kwenda kwenye mfumo wa 4-4-2, ambapo pembeni kulia alicheza Juma Mahadhi na kushoto alicheza Emmanuel Martin ambapo mbele walicheza Pius Buswita na Obrey Chirwa aliyecheza kama mshambuliaji wa kati huku Pius Buswita akicheza kama mshambuliaji wa pili.
Hii ilimpa uhuru Pius Buswita kuwa anashuka katikati na kwenda pembeni, kitu ambacho kiliisaidia Yanga kwani alipokea pasi akiwa pembeni na kutengeneza goli la kwanza.
Ingizo la Juma Mahadhi lilikuwa chachu kubwa eneo la kulia kwani alileta uhai eneo lile. Kipindi cha kwanza Yanga walijaribu sana kutumia mipira mirefu na kupitia pembeni lakini walikosa watu ambao wangetengeneza magoli kupitia pembeni.
Lakini Juma Mahadhi aliongeza hiki kitu ambacho kipindi cha kwanza hakikuwepo mpaka akasababisha goli la pili.
Kadi nyekundu ya golikipa wa Njombe mji iliwarudisha nyuma sana Njombe mji na ilikuwa msaada mkubwa kwa Yanga ambayo haikuwa na mzigo tena wa kushambuliwa na wenyewe wakawa na nguvu kubwa ya kushambulia mpaka wakafanikiwa kushinda magoli manne (4).