Sambaza....

Kuna kitu kimoja ambacho mashabiki wa Simba wanatakiwa kukifanya kwa dhati ya moyo wao wote bila unafiki. Nacho ni kusimama kifua mbele na kuwapongeza wachezaji wa Simba bila uoga. Hawa ndiyo mashujaa wao kwa msimu huu.

Mashujaa ambao wametoa kwenye ukame na kuwapeleka kwenye mvua kwa ajili ya kulima chakula ambacho ƙkitawapa nafasi wao kula na kunenepa.

Hapana shaka kwa sasa shabiki pekee mwenye afya ya moyo, shabiki ambaye amenenepa mwili mpaka moyo ni shabiki wa Simba.

Huyu ndiye mwenye afya iliyobora kuzidi shabiki yeyote hapa nchini na hii ni kwa sababu ya wachezaji wao wamewapeleka sehemu ambayo ina chakula.

Wamewatoa sehemu yenye njaa, sehemu yenye mateso, sehemu ya huzuni na masikitiko na kuwapeleka sehemu yenye furaha kwa muda mwingi.

Sehemu ambayo kuna robo fainali ya ligi ya mabingwa barani Afrika. Yani vilabu nane pekee vimebaki pamoja na Simba kwenye michuano hii.

Unaionaje hii hatua ?. Unadhani ni hatua ya kubeza hata kidogo ?. Bila shaka jibu ni hapana. Hii ni hatua kubwa sana kwa Simba.

Hii ni hatua ambayo hata wao mashabiki walikuwa hawategemei ƙkabisa kama watafika. Hii ni sehemu yenye hadhi kubwa sana.

Na sidhani kama Simba lengo lao lilikuwa kufika hatua hii. Ukimsikiliza tajiri wa Simba, Mohamed Dewji kuna kitu huwa anakirudia sana tena mara kwa mara.

Simba imevuka lengo. Hii ni kauli ambayo huwa inatoka sana kwenye kinywa cha tajiri huyo kijana barani Afrika.

Ni kauli ambayo huwezi kusita kusema kuwa hapo walipofikia Simba wanahitaji sana pongezi. Nilitegemea sana kabla ya mchezo mashabiki wangesimama kuwakaribisha mashujaa wao kwa makofi.

Nilitegemea hivo hivo baada ya mchezo mashabiki hawa wangesimama na kuwapigia makofi wachezaji wa Simba na kusema Asante.

John Bocco akiwa katika harakati za kutafuta ushindi nyumbani

Asante kwa shibe hii ya mafanikio. Asante kwa nafasi hii kubwa ambayo imewajengea heshima kubwa sana barani Afrika.

Asante kwa kufanikiwa kuvuka kundi ambalo lilikuwa na makamu bingwa wawili wa mashindano ya CAF msimu uliopita.

Yani Simba kwa kifupi ilikuwa na As Vita kwenye kundi moja. Huyu ni makamu bingwa wa kombe la shirikisho msimu jana.

Simba ilikuwa na Al Ahly, huyu ni makamu bingwa wa ligi ya mabingwa barani Afrika msimu jana akifungwa na Esperance huku As Vita akifungwa na Wydad.

Huyu Al Ahly ndiye bingwa wa kihistoria wa ligi ya mabingwa Afrika. Inawezekana kabisa Souara anaweza kuonekana wa kawaida lakini hawa vigogo wawili (Al Ahly na As Vita ) walikuwa wanaume haswaaa.

Watu ambao mashindano haya ya vilabu Afrika wanayaona kama yao. Ndiyo watu hao hao ambao Simba iliweza kujipenyeza katikati yao.

Kuna chochote cha kuwasifu hawa vijana zaidi ya kuwaita mashujaa?. Ni mashujaa haswaa. Wamefika sehemu ambayo wengi hawakutegemea.

Tena wakiongozwa na John Bocco, nahodha. Nahodha ambaye ni imara na mhimili mkubwa wa Simba katika michuano hii.

Huyu ndiye aliwaongoza ipasavyo wanajeshi wote wa Simba katika uwanja wa vita mpaka kufikia hatua hii.

Mashabiki wa Simba Sc

Huyu ndiye aliyeunda utatu mtakatifu,utatu ambao ulikuwa na ukatili kwa mabeki wa timu pinzani. Utatu wa Kagere , Okwi na yeye.

Huyu ndiye ambaye alikuwa na uwezo mkubwa wa kufunga magoli na kupika magoli katika michuano hii ndani ya ƙkikosi cha Simba.

Huyu ndiye ambaye aliwapa moyo wachezaji wa Simba kipindi ambacho walikata tamaa uwanjani, akitumia cheo chake cha unahodha.

Huyu ndiye ambaye alikuwa anazunguka sana eneo la mbele kwa kuhakikisha anakabia juu kuhakikisha mabeki wa timu pinzani wasiwe huru kuanzisha mashambulizi.

Kwa kifupi John Bocco alikuwa mtu muhimu sana ndani ya kikosi cha Simba kwenye michuano hii. Anastahili sana pongezi kubwa mpaka kufikia hapa.

Anastahili sana heshima yake. Ndiyo maana naendelea kusisitiza kuwa mashabiki wa Simba wanatakiwa kusimama na kuwapongeza wachezaji hata kama wakitolewa.

Simba inatakiwa kupokelewa kishujaa pale kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa mwalimu Julius Kambarage Nyerere hata kama wakitolewa.

Maandamano yanatakiwa kuandaliwa ili kuwapokea hawa mashujaa wetu kwa msimu huu. Tusiwatenge kabisa.

Tusiwalaumu kabisa. Najua jana John Bocco alikosa nafasi tatu za wazi ikiwemo penati. Nafasi ambazo zinaweza kumgombanisha na mashabiki.

Lakini mashabiki wanatakiwa kuelewa hivi vitu hutokea sana kwenye mpira na kwa mafanikio haya ya Simba kila mchezaji anastahili makofi na siyo lawama. John Bocco anastahili kupongezwa sana kuliko kulaumiwa.

Sambaza....