Fikiria neno “hatua” ni neno dogo lakini ndilo limebeba tafasri halisi ya neno maendeleo.
Maendeleo ni wingi wa hatua zinazopigwa kimahesabu, haijalishi ukubwa wa hatua ambazo mtu anapiga cha muhimu ziwe hatua za kwenda mbele.
Katika safari ya maisha ni ngumu kuanzia hatua ya tano bila kuanza hatua ya kwanza. Ndipo hapo wengi wetu huwa tunajisahau sana.
Na wakati mwingine huwa tunajifariji sana, kitu ambacho siyo kweli, ndiyo maana huwezi kushangaa kila jina la kocha mpya wa timu ya Taifa “Taifa Stars” watu wengi hujaa matumaini makubwa sana.
Wengi wetu huwa tunamchukulia kocha huyo kama mkombozi wa soka letu na kusahau kuwa kuna hatua nne tumeziruka.
Mimi ni mmoja ya watu ambao huwa siamini katika mafanikio ya timu ya Taifa kupitia vyeti vikubwa vya kocha wa timu Taifa ilihali mkondo wetu wa kuzalishia wachezaji watakaokuja kucheza timu ya taifa ni mbovu.
Tunajisahau wapi pa kuanzia kabla hatujafika kuwekeza matumaini yetu kwa makocha wa kigeni wenye vyeti vya kuvutia.
Hakuna kitu tutakachonufaika nacho wakati tuna makocha wenye vyeti vya hali ya juu wakati ligi yetu ikiendeshwa katika mazingira ambayo siyo rafiki kuzalisha timu imara ya Taifa.
Mazingira ambayo waamuzi wengi wanafanya makosa mengi ambayo yanazigharimu timu nyingi. Mazingira ambayo ratiba ya ligi inakuwa rafiki kwa timu fulani huku timu zingine zikiwa wahanga wa ratiba husika.
Mazingira ambayo viwanja vinavyotumika kwa ajili ya kuchezea ligi kuu haviendani na vyeti vya kocha wa timu ya Taifa.
Hakuna jitihada kubwa ambazo zinafanywa na viongozi wa TFF kuwashawishi wamiliki wa viwanja husika angalau kukarabati maeneo ya kuchezea ya viwanja husika.
Imekuwa jambo la kawaida sana ligi yetu kuchezewa kwenye nyasi ambazo hazina viwango vya juu. Nyasi ambazo zinanyima ubunifu wa wachezaji husika na hata mbinu za makocha wengi.
Ni bora tufikirie kuboresha ligi zetu ziwe zinaendeshwa katika mazingira ambayo ni bora, mazingira ambayo yatakuwa na uwezo wa kuzalisha wachezaji bora ambao watakuwa siyo mzigo kwa makocha ambao wanaletwa kufundisha timu ya Taifa.
Wachezaji wetu wamekulia malezi ambayo hayawaandai kuwa wachezaji wa kulipwa. Wanakosa vitu vingi sana ambavyo walitakiwa kuvipata wakati wakiwa na umri mdogo.
Ndipo hapo suala la mpira kuanzia kuchezwa kwenye umri mdogo unapoanzia. Jitihada za kuwa na vituo vya kulea, kukuza na kuibua vipaji zinapohitajika.
Tunatakiwa tumtengeneze mchezaji atakayekuja kucheza timu ya Taifa tangu akiwa mtoto mdogo.
Mchezaji huyu aandaliwe vizuri na awe na njaa ya yeye kufika mbali. Awe na njaa ya kucheza nje ya nchi kwenye ligi bora.
Tumekuwa tukikosa wachezaji wa kulipwa kwenye timu yetu ya Taifa. Wachezaji hawa wanafaida kubwa sana kwetu sisi kwenye maendeleo ya mpira wetu kwa sababu wamezoea ligi za ushindani hivyo ni rahisi kwetu sisi kushindana kwenye mashindano yanahusu timu za Taifa.
Tusifikirie sana kuhusu kupata makocha wa daraja la juu kwenye timu ya Taifa na kusahau kuwa tushawahi kuwa na makocha wa daraja la juu lakini hakuna sehemu ambayo tulifanikiwa kufika.
Turudi katika kutengeneza msingi imara, na kuachana na habari za kuweka paa zuri na bora ilihali msingi wa nyumba yetu ni mbovu.